Wakenya walifanya maandamano Januari 2024 kupinga mauaji ya wanawake nchini humo.  / Picha: Reuters

Serikali ya Kenya imetoa agizo kwa wamiliki wa nyumba za wageni zinazokodishwa kwa muda mfupi maafuru Airbnb kusajili biashara hizo kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Utalii nchini humo.

"Kuanzia Februari 5, 2024, maafisa wa serikali pamoja na maafisa wa Mamlaka ya Udhibiti wa Utalii wataanza kukagua maeneo yote ambayo yatakuwa yamesajiliwa," taarifa ya serikali imesema.

Airbnb ni soko la mtandaoni ambalo huunganisha wamiliki wa nyumba pamoja na wateja wanaotaka kukodisha kwa muda mfupi.

Airbnb imekuwa ni sehemu kubwa ya wananchi kujiongezea kipato kupitia mali zao. Huku wageni wakiona utaratibu wa kukodi nyumba hizo ni wa bei nafuu ikilinganishwa na hoteli.

Maagizo mapya yanayotolewa na serikali ya Kenya yanafuatilia mauaji ya wanawake wawili mwezi Januari mwaka huu katika maeneo ya malazi ya kukodisha.

Katika eneo moja, moja ya nyumba hizo haikuwa na kamera ya CCTV hivyo kufanya ukusanyaji wa ushahidi wa mauaji kuwa mgumu.

"Pia tutawasiliana na majukwaa ya kusajili malazi (ambapo watu huenda kutafuta maeneo hayo mitandaoni) na kuhakikisha zile nyumba ambazo hazijasajiwa na serikali haziwekwi katika majukwaa hayo," imeongeza kusema taarifa hiyo.

Serikali pia inatishia kutoa adhabu kali ikiwa ni pamoja na faini na kufutwa kwa nyumba hizo katika majukwaa hayo mitandaoni iwapo watashindwa kutimiza masharti.

TRT Afrika