Siku ya Jamhuri ni sikukuu ya kitaifa nchini Kenya, inayoadhimishwa kila tarehe 12 Disemba/ Picha Rais William Ruto X 

Kenya imeadhimisha miaka 61 tangu kuwa Jamhuri.

Siku ya Jamhuri ni sikukuu ya kitaifa nchini Kenya, inayoadhimishwa tarehe 12 Disemba kila mwaka.

Hiyo ndiyo siku rasmi ambayo Kenya ilipata kuwa nchi huru mnamo Disemba 12, 1963, miezi sita na siku kumi na moja baada ya kupata utawala wa ndani mnamo 1 Juni 1963 (Siku ya Madaraka) kutoka Uingereza.

Kenya baadaye ikawa Jamhuri, na kuapishwa kwa Jomo Kenyatta kama Rais kulifanyika tarehe 12 Disemba 1964, mwaka mmoja kamili baada ya Kenya kupata uhuru mwaka 1963.

Kenyatta, akiwa ameapishwa awali kama Waziri Mkuu, aliendelea kuwa Waziri Mkuu wa Kenya mpya, kabla ya kushika wadhifa wa rais mwaka mmoja baada ya Siku ya Uhuru.

Rais William Ruto alichukua fursa hii kukashifu kile alichoita upinzani potofu Photo by William Ruto on X

"Leo tunathibitisha kwa kutafakari yale tuliyotimiza tangu kuinua bendera ya taifa letu, kwamba kwa kubaki waaminifu kwa utambulisho wetu wa kitaifa, tumebaki thabiti katika misimu ya wingi na uhaba," rais Willim Ruto alisema akiongoza sherehe za kuadhimisha siku hii katika uwanja Uhuru Gardens jijini Nairobi.

"Katika wakati wetu, kizazi chetu hakipaswi kamwe kusahau tulipokuwa miongo sita iliyopita. Hatupaswi kupuuza ukweli kwamba uhuru, demokrasia na maendeleo yetu yalipatikana kupitia michango ya mamilioni ya wazalendo waliodhamiria," Rais Ruto aliongezea.

Rais wa Gambia Adama Barrow alikuwa mgeni rasmi katika sherehe hizo.

"Tangu uhuru, Kenya imeendelea kuongoza katika utawala wa kidemokrasia, amani na usalama. Kama mhusika mkuu katika ushirikiano wa Afrika, mbinu za nchi katika mabadiliko ya hali ya hewa na maendeleo hutumika kama mfano kwa wengine."

Rais Ruto alichukua fursa hii kukashifu kile alichoita upinzani potofu.

"Ninakaribisha kukosolewa na kusikiliza maoni ili kujifunza na kuboresha. Hata hivyo, upinzani mara nyingi hutegemea taarifa ambazo hazina usahihi," alisema.

Rais alitetea sera zake akisema kuwa zina nia njema ya kuboresha maisha licha ya upinzani wa watu.

"Ni ukweli kwamba gharama za bidhaa za msingi na mfumuko wa bei umepungua. Wakosoaji watasema nini tunapoanza kutoa funguo kwa wamiliki wapya wa nyumba za bei nafuu?" aliuliza.

Kwa saa Kenya inakabiliwa na gharama ya juu ya maisha, ukosefu wa ajira, kukosekana kwa usalama wa kutosha, na wakati huo huo uongozi wa Rais Ruto umejipata lawamani kutokana na changamoto hizo.

TRT Afrika