Wizara ya Elimu nchini Kenya imeagiza kufanywa ukaguzi wa shule zote za bweni kutathmini utekelezwaji wao wa viwango vya usalama kufuatia visa 107 vya moto shuleni na vingine zaidi ya 200 vya fujo tangu Januari.
Waziri wa Elimu Julius Migos alifichua kuwa kati ya visa 107 vya moto, 36 vimetokea katika muhula wa tatu na hasa vikilenga shule za bweni.
"Tangu Januari, 2024 hadi Septemba 16, 2024, kumekuwa na visa 107 vya moto katika shule zetu, huku 36 kati ya hizi zikitokea katika Muhula huu wa Tatu," Migos aliwaambia wabunge Jumanne.
Ukaguzi utaarifu hatua zinazohitajika kwa shule zote mbili kulikotokea vifo na maafisa wanaoendesha kesi za kutofuata sheria.
Hii inakuja baada ya agizo la Rais WIlliam Ruto mnamo Septamba 11, kufanywa ukaguzi wa usalama katika shule zote baada ya tukio la moto katika baadhi ya shule nchini humo.
Rais Pia aliwataka wakuu wa wizara ya elimu, idara ya ujasusi na wadau wengine wote kuharakisha uchunguzi kwa kilichosababisha moto katika shule ya Endarasha, iliyowaua watoto 21.
Wito huo wa Rais umekaririwa tena Jumanne na spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetangula wakati wa kikao cha maswali bungeni na waziri wa elimu.
''Sijui ni nini mnafanya kama wizara. Katika miaka ya nyuma kulikuwa na hatua za mara moja zinachukuliw akama kuzifunga shule nakufuta leseni ya shulehizo kunapotokea mkasa kama huu, hilo halijafanyika hapa,'' alisema Spika Wetangula. 'Lakini ni muhimu tupate uwajibikaji wa kihalifu au uzembe kwa wahusika,'' aliongeza.
Lakini waziri alijibu kusema kuwa bado wanasubiri uchunguzi ukamilike kabla ya kuchukua hatua.
''Iwapo kuna yeyote, wakiwemo maafisa wa wizara yetu ambao hawakutekeleza wajibu wao, tutachukua hatua kamili dhidi yao,'' alisema waziri Migos.
Mnamo Septemba 6, moto uliteketeza bweni la wanafunzi katika shule ya Hillside Endarasha na kuwauwa watoto 21. wengi wao walioteketezwa kupindukia.
Wadau wengi wameelekezea serikali lawama kwa kukosa kuweka mikakati yakiusalama muafaka ya kulinda wanafunzi shuleni.