Uharibifu wa mali katika maandamano unakisiwa kugharimu zaidi ya dola Milioni tano Picha : Twitter Kithure Kindiki

Zaidi ya watu 300 akiwemo mbunge mmoja wamekamatwa na polisi nchini Kenya kuhusiana na maandamano yaliyoishia kwa ghasia na maafa Jumatano.

Waziri wa usalama wa ndani wa Kenya Kithure Kindiki amesema kuwa washukiwa hao watafunguliwa mashtaka mbali mbali ikiwemo uharibifu wa maliya umma na kuvuruga amani.

Miongoni mwa waliokamatwa ni mbunge wa eneo la Mavoko Patrick Makau ambaye anatuhumiwa kuhusika ama kuchochea uharibifu wa barabara kuu ya Expressway.

"Tutawakamata, tutawatia nguvuni, na kuwafungulia mashtaka wale wote waliohusika katika ghasia na uharibifu wa jana," Alisema waziri Kindiki. ''Tayari 316 wamekamatwa.'' aliongeza.

Haya yamejiri wakati waziri wa usafiri Kipchumba Murkomen akisema kuwa uharibifu katika barabara kuu ya Express jijini Nairobi unakisiwa kufikia dola milioni tano.

Utumiaji mbaya wa silaha

Waziri wa usalama wa ndani Kithure Kindiki pia alitangaza kuwa viongozi wanaohusishwa na maandamano hayo wataondolewa ulinzi na kupokonywa silaha wanazo miliki.

“Hatuwezi kuwa na waandamanaji wenye silaha. Hii inatumika kwa kila mtu anayeshiriki katika maandamano, ikiwa ni pamoja na walinzi,'' alisema Waziri Kindiki. ''Hatutaruhusu silaha, hata kwa wale wanaoshiriki maandamano ya amani,” alieleza.

Watu 6 walifariki Jumatano katika maandamano yaliyoitishwa na muungano wa Upinzani Azimio, Picha : Reuters

Kindiki alikariri kuwa serikali haiwezi kuruhusu maandamano yoyote yanayotishia usalama wa raia na kusababisha uharibifu wa mali.

Watu 6 walifariki Jumatano katika maandamano yaliyoitishwa na muungano wa Upinzani Azimio, kulalamikia kuongezeka kwa gharama ya maisha na kupinga sheria ya fedha iliyopitishwa na bunge.

Viongozi wa Azimio (Muungano wa Upinzani) wanadai kuwa sheria hiyo inawakandamiza raia kwa kuongeza kodi wanayotozwa.

Kiongozi wa Muungano huo Raila Odinga alitangaza Jumatano kuwa amesitisha maandamano kwa kuhofia maafa zaidi ya raia, japo baadhi ya viongozi wengine wa Azimio walinukuliwa Alhamis kusema kuwa wataendelea na maandamano kwa siku tatu kila wiki kuanzia wiki ijayo.

TRT Afrika