Takriban watu kumi wanahofiwa kufariki katika eneo la Bonde la Ufa nchini Kenya baada ya lori kugonga magari kadhaa mnamo Juni 30. Picha: Reuters

Shirika la msalaba mwekundu Kenya limetoa wito kwa wananchi kuchangia damu kuwaokoa waliaothiriwa katika ajali Ijumaa .

Jumla ya magari tisa yalihusika katika ajali hiyo likiwemo lori lililopoteza mwelekeo na kuyagonga magari na angalau matatu nne.

"Tujumuike pamoja tuwasaidie ndugu na dada zetu wenye shida," taarifa yake katika mtandao wa Twitter umesema.

Lori hilo pia liliwagonga wachuuzi waliokuwa wakiuza chakula pembeni ya barabara.

Idadi ya waliofariki kutokana na ajali hiyo imeongezeka hadi 52 kufikia Jumamosi.

Manusura 30 wamelazwa katika hospitali za Kericho na Nakuru.

"Changia damu kwa ajili ya majeruhi wa Londiani MCI katika Hospitali ya Rufaa ya Kericho, Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Londiani au hospitali yoyote ndani ya Kaunti ya Kericho."

Waziri wa Mambo ya Ndani na tawala wa Kitaifa Kithure Kindiki amewataka Maafisa wa polisi kote nchini kutekeleza sheria za trafiki kwa uthabiti.

"Polisi wakamate wahalifu wote wanaokiuka sheria za trafiki, ikiwa ni pamoja na wale wanaoendesha magari mabovu na yasiyofaa barabarani," Kindiki amesema katika taarifa.

Ajali ya Ijumaa

Kamanda wa Polisi Kaunti ya Kericho Geoffrey Mayek alithibitisha vifo hivyo katika hotuba yake kwa wanahabari Ijumaa jioni.

Afisa Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Londiani, Agnes Kunga, alisema ajali hiyo ilitokea saa 12:30 jioni saa za Kenya, na juhudi za uokoaji zinaendelea.

Ripoti zinaonyesha kuwa dereva wa lori alipoteza udhibiti na kugonga magari mengine sita, na kuwajeruhi watu kadhaa na wengine kuhofiwa kufariki.

"shingo ya lori ilipoteza muelekeo na dereva akashindwa kuimudu, ikisababisha ajali mbaya ambayo ilihusisha magari mengi," Huduma za Dharura za Tiba za Kenya zilisema kwenye Twitter.

Walioshuhudia walisema kuwa waendeshaji wa pikipiki na watembea kwa miguu ni miongoni mwa waliojeruhiwa katika ajali hiyo, siku ya Ijumaa.

Londiani, kilomita 220 kaskazini magharibi mwa mji mkuu wa Kenya, Nairobi, ni eneo hatari ambalo limechukua maisha ya watumiaji wengi wa barabara hapo awali.

TRT Afrika