Wizara ya Elimu nchini Kenya imebatilisha ada za chuo kikuu zilizotumiwa awali kwa kundi la KCSE la 2023.
Uamuzi huu ulifanywa baada ya malalamiko ya umma na mkanganyiko kuhusu muundo mpya wa ada.
Katika taarifa yake ya Julai 19, Katibu Mkuu wizara ya elimu Beatrice Inyangala alisema muundo huo mpya utatolewa kuanzia Agosti 5.
Inyangala aliwashauri wazazi kupuuza mawasiliano ya awali kutoka kwa taasisi hizo.
“Wizara ya Elimu inapenda kuwafahamisha Umma, hususan wazazi na walezi wa wanafunzi kuwa ada zinazopaswa kulipwa na wanafunzi na familia zao kuhusiana na gharama kamili za kila programu ya shahada kama ilivyoelezwa hapo awali katika barua za udahili zinabatilishwa na haitatumika tena," Inyangala alisema.
Licha ya mabadiliko ya ada, upangaji wa wanafunzi katika programu zao za masomo utaendelea kwa mujibu wa ratiba.
Madai ya kutojali
Hatua ya serikali inalenga kushughulikia wasiwasi juu ya gharama ya elimu ya chuo kikuu na kuhakikisha uwazi katika mtindo wa ufadhili.
Katika jibu lake kwenye mtandao wa X, seneta wa Busia, Magharibi mwa Kenya Okiya Omtata alikashifu mpango wa serikali kuongeza ada bil akuwajali wanafunzi.
''Mtindo mpya wa ufadhili wa Vyuo Vikuu ulitungwa kwa upotofu mkubwa. tunatakiwa kurejea mtindo wa awali kwa wanafunzi wanaoendelea na wapya na hatimaye tuweze kuondoa kabisa ada ya masomo kwa wanafunzo wa viwango vyote vya masomo,'' alisema Omtata.
Awali kamati ya ofisi ya Rais kuhusu Marekebisho ya Elimu ilipendekeza ongezeko kubwa la 225% ya ada zinazolipwa na wanafunzi wanaofadhiliwa na serikali katika vyuo vikuu vya umma.
Kwa sasa, wanafunzi hawa wanalipa Ksh. 16,000 kwa ada ya masomo, na nyongeza iliyopendekezwa ingeongeza kiasi hiki hadi Ksh. 52,000 kwa mwaka kwa kila mwanafunzi.
Kwa mujibu wa kamati hiyo, wazo lao lilikuwa ni kwamba ongezeko la ada litavipatia vyuo vikuu fedha wanazohitaji ili kuboresha vifaa na rasilimali zinazohitajika kwa wanafunzi.
Kumudu gharama
Kwa miaka mingi tatizo la wanafunzi kushindwa kumudu gharama ya juu ya elimu iliwasababisha wengi kutoendelea na masomo ya vyuo, isipokuwa wanaotoka familia za kitajiri, wanaobahatika na nafasi chache za ruzuku ya serikali ya masomo au kutegemea michango ya jamii.
Baadhi ya wazazi walilazimika kuuza mali zao ikiwemo mashamba, mifugo na nyumba ili kugharamia masomo ya juu ya watoto wao.
Mfumo wa elimu ya juu nchini Kenya unakabiliwa na changamoto mbalimbali, kama vile ufadhili mdogo, uhaba wa rasilimali na vifaa.
Mnamo 1995, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HELB) ilianzishwa ili kutoa mikopo kwa wanafunzi ambao hawakuweza kumudu ada ya masomo.
Tangu 1991, ada za masomo zimehifadhiwa kwa kiasi cha kawaida cha Ksh 16,000 kwa muhula. Pendekezo la hivi majuzi la kuongeza ada ya masomo hadi Ksh 52,000 kwa muhula ni ongezeko la kwanza kubwa tangu 1991.
Mnamo 2015, Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) yalipitishwa na nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa kama wito wa wote wa kuchukua hatua kukomesha umaskini, kulinda mazingira na kuhakikisha kuwa watu wote wanafurahia amani na ustawi ifikapo mwaka 2030.
Lengo la Maendeleo Endelevu nambari 4, linalenga kuhakikisha elimu bora iliyo jumuishi na yenye usawa na kukuza fursa za kujifunza maishani kwa wote. Lengo hili linasaidia kupunguza tofauti na ukosefu wa usawa katika elimu, katika suala la upatikanaji na ubora.
Mfumo huo mpya wa ufadhili uliharakishwa na kabla ya wakati wake, na kuhamisha jukumu la kutoa elimu kutoka kwa serikali kwa wazazi, ambao wengi wao wanatatizika kuwaweka watoto wao shuleni,'' alisema Seneta Omtata. ''Maana yake imewafanya wanafunzi wengi kughairi semesta, kuacha shule au kutoweza kuripoti Chuo Kikuu kabisa,'' alilalamika Seneta huyo, ambaye pia nimwanaharakati wa haki za binadamu nchini Kenya.