Madaktari na wataalamu wengine wa afya wanaitaka serikali kutimiza mahitaji yao, la sivyo wataendelea na mgomo wao na kudumaza kabisa huduma ya afya nchini./ Picha : Reuters 

Jeshi la polisi nchini Kenya limetoa onyo kali kwa madaktari wanaogoma likisema kuwa mgomo huo umegeuka kuwa usumbufu kwa amani na usalama wa taifa.

Katika taarifa iliyochapisha katika mtandao wa X, zamani twitter, jeshi la polisi lilisema kuwa madaktari na maafisa wa kliniki wanaoshiriki mgomo wamekuwa wakisababisha zahma katika mahospitali, barabara na maeneo ya umma na kusababisha fujo zisizo na maana.

''Madaktari wamekuwa kero kwa umma, kupiga kelele za firimbi na vuvuzela wakati wa maandamano hivyo kusababisha usumbufu kwa wagonjwa hospitalini na umma kwa ujumla'', imesema taarifa hiyo.

Polisi pia wanasema wamepokea malalamiko kuwa madaktari hao wamekuwa wakizuia wafanyakazi wengine kuendelea na shughuli zao.

Mgomo usio halali

''Jeshi la polisi limeshuhudia na kupokea malalamiko ya kero zilizotokana na mgomo huo huku madaktari wakilala njiani hivyo kukwamisha usafiri katika barabara kuu, barabara za umma na kukwamisha mtiririko wa magari na usafiri wa watu'' ilani hiyo iliendelea kusema.

Katika kukabiliana na malalamiko hayo, Inspekta mkuu wa polisi Japhet Koome amesema kuwa makamanda wote wameagizwa kudhibiti hali kwa nguvu zote kwa mujibu wa sheria.

Inspekta mkuu huyo amesema kuwa wamepata taarifa kuwa baadhi ya wakora wanajiingiza ndani ya maandamano hayo kuhatarishia watu maisha na kupora mali za watu.

Pia amesema maandamano yanayofanyika katika sehemu nyingi hayakupewa vibali vya kuendelea.

Muungano wa Madaktari, Wafamasia na Madaktari wa Meno nchini Kenya, KPMDU, uliipa serikali notisi ya mgomo kutoka tarehe Machi 13, 2024, ikiwa serikali itashindwa kutatua changamoto zao.

Madaktari hao wanaitaka serikali kuwatuma kazini wanafunzi wahudumu wa afya mara moja na kufuta malimbikizo ya mishahara ya madaktari kulingana na Makubaliano ya Pamoja ya 2017.

"Hayo ni mambo ambayo yanafaa kutekelezwa,” Katibu Mkuu wa Muungano wa Madaktari wa Meno wa Kenya Davji Atellah alisema wiki jana.

Madaktari na wataalamu wengine wa afya wanaitaka serikali kutimiza mahitaji yao, la sivyo wataendelea na mgomo wao na kudumaza kabisa huduma ya afya nchini.

Wahudumu wa afya ambao wamehudumu kwa miaka minne chini ya kandarasi katika taasisi za afya ya umma wanadai ajira ya kudumu ambayo walikuwa wamehakikishiwa na serikali ya Kenya kufuatia miaka mitatu ya huduma.

TRT Afrika