Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergey Lavrov / Picha: AA

Rais wa Kenya William Ruto amesema biashara kati ya Kenya na Urusi bado iko chini licha ya uwezo mkubwa. Alisema alipokuwa akikutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergey Lavrov aliyewasili nchini Kenya siku ya Jumatatu akiwa ameungana na wajumbe wengine.

Ruto amesema "nchi hizo mbili zitatia saini mkataba wa kibiashara ambao utaipa biashara msukumo unaohitajika."

Viongozi hao wawili walikubaliana juu ya haja ya kulifanyia mageuzi Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ili kulifanya kuwa mwakilishi zaidi na kuitikia mahitaji ya Karne ya 21.

Rais Ruto alisema Afrika inapaswa kuwakilishwa katika baraza la usalama, chombo kikuu cha Umoja wa Mataifa cha kufanya maamuzi.

"Bara linaweza kuleta mezani mawazo ya thamani, mapendekezo na uzoefu ambao utaitumikia dunia vyema," rais alieleza.

Lavrov pia alikutana na ungozi wa bunge la taifa la Kenya.

Waziri wa mambo ya nje Sergei Lavrov alikutana na spika wa bunge la Kenya Moses Wetangula jijini Nairobi

Lavrov alikuwa Nairobi akielekea kwenye Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa wa BRICs mjini CapeTown, Afrika Kusini.

Afrika Kusini ni mojawapo ya nchi tano zilizoungana na Urusi chini ya muungano maarufu kama BRICS kwa ajili ya kulenga maendeleo ya kiuchumi . BRICS ni kifupi cha nchi tano zinazoinukia kiuchumi: Brazili, Urusi, India, China na Afrika Kusini.

Ziara yake iko katika msingi wa ziara yake ya Afrika katika jitihada za kuimarisha uhusiano kati ya Urusi na Afrika.

Je, kwa nini Urusi inafanya ziara nyingi barani Afrika?

Tangu mwaka huu uanze Urusi imefanya takriban ziara saba barani Afrika.

Wataalamu wa kisiasa wanasema Moscow imekuwa na nia ya kuanzisha tena uhusiano wake wa zamani wa Kisovieti na mataifa ya Kiafrika na kuongeza ushawishi katika bara hilo.

Inajionyesha kama njia mbadala ya mataifa yanayoonekana kuwa na "maslahi binafsi" kama vile Uingereza na Marekani.

Kwa mfano Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Lavrov alitembelea Eritrea, nchi katika pembe ya Afrika ambayo imetengwa kidiplomasia na kwa usaidizi na Marekani na nchi za Ulaya.

"Tuko tayari kukidhi mahitaji ya Eritrea kuhusu kudumisha uwezo wake wa ulinzi, na bila shaka tutakuwa tukishirikiana katika masuala ya kibinadamu. Tuko tayari kuongeza idadi ya ufadhili wa masomo ambayo Waeritrea hupokea kila mwaka kutoka kwa Serikali ya Urusi."

Wakati Wizara ya Mambo ya nje kutoka Somalia ilivyotembelea Urusi mwezi Mei mwaka huu Urusi ilisema kuwa "inaheshimu Afrika" .

Urusi na Afrika Kusini zipo katika muungano wa kiuchumi maarufu kama BRICS ambapo nchi tano zimeungana kwa ajili ya kuinuka kiuchumi

"Siku zote tumekuwa tukiamini kwamba Waafrika lazima watatue matatizo yao kwa kuzingatia maamuzi na maelewano yao wenyewe," Lavrov alisema wakati ujumbe wa Somalia ulpoitembelea Urusi Mwezi Mei.

"Ni muhimu kuchukulia kwa uzito ukweli kwamba Afrika ina haki kamili ya kutatua matatizo yake kwa kujitegemea na kuchukua jukumu kubwa kama kituo katika mpango wa ulimwengu wa pande nyingi," Lavrov aliongezea.

Ukraine yamenyana na uhusiano wa Urusi na Afrika

Huku Urusi ikiongeza juhudi zake za kuleta bara la Afrika karibu , Ukraine nayo imeanza kampeni ya kuzivutia nchi za Afrika . Uhusiano kati yake na Afrika ipo chini ikilinganishswa na ile kati ya Urusi na Afrika.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Dmytro Kuleba naye alizuru Afrika, akianza na Makao Makuu ya Umoja wa Afrika jijini Addis Ababa nchini Ethiopia.

Ukraine inasema inalenga kuidhinisha mfumo wa amani wa Rais Volodymyr Zelensky na kuhakikisha usambazaji wa nafaka katika nchi za Afrika.

" Tunajitahidi kufanya mazungumzo yetu yawe ya kimfumo zaidi na ya mara kwa mara, ili Ukraine na nchi za Afrika zielewane vizuri zaidi," alisema.

"Hivi majuzi tumepitisha mkakati wetu wa kwanza wa Kiafrika na kuimarisha mazungumzo yetu ya kisiasa na nchi nyingi katika bara hili," Waziri wa Mambo ya Nje Dmytro Kuleba alisema katika taarifa yake kuadhimisha miaka 60 ya kuanzishwa muungano wa Umoja wa Afrika.

Mbali na uhusiano wa kidiplomasi na Afrika , nchi hizi mbili zinazong'ang'ania kutambuliwa zaidi na Afrika ni chanzo cha nafaka na mbolea kwa nchi nyingi za Afrika.

Nchi za Afrika hazijaongea kwa sauti moja katika kura za kutetea Urusi au Ukraine katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.

Huku nchi zingine zimeunga mkono Urusi au Ukraine , zingine zimewapinga na zingine kuamua kutoegemea upande wowote.