Wizara ya elimu nchini Kenya imesema itaunda mahakama maalum itakayosikiliza kesi za wanao husika na udanganyifu katika mitihani ya kitaifa.
Katika ujumbe wake wakati wa uzinduzi wa mitihani ya kitaifa kwa wanafunzi wa gredi ya 6 nchini, Waziri wa Elimu alitoa onyo kali kwa yeyote atakayekutwa na kosa la udanganyifu kuwa atachukuliwa hatua ikiwemo kifungo.
''Wizara yangu itashirikiana kwa karibu na mfumo wa haki ya jinai kuunda mahakama maalum ambazo zitashughulikia kesi mahususi zinazohusiana na udanganyifu wa mitihani ya kitaifa,'' alisema Julius Ogamba, Waziri wa elimu nchiin Kenya.
Waziri Ogamba pia amesema kuwa kesi hizo zitaharakishwa kusikilizwa na hukumu kutolewa mapema.
''Tumeomba kuwe na vikao maalum vya mahakama ili kesi za makosa ya mitihani zisikilizwe na kuamuliwa ndani ya miezi mitatu,'' alisema Ogamba.
Kumekuwa na visa vya udanganyifu katika mitihani nchini Kenya huku wengi wakilaumu utamaduni wa ushindani mkali sio tu kati ya wanafunzi bali kati ya shule
Hii imesababisha wakati mwingine walimu na wasimamizi wa elimu za mikoa kuhusika na udanganyifu kwa ari ya kutafutia matokeo bora shule zao.
Waziri amesema kuwa miongoni mwa mabadiliko walioleta ili kupunguza udanganyifu huo ni kubadili mfumo wa kuwapandisha vyeo walimu wakuu wa shule.
''Tunataka kukuza wananchi waliobobea pande zote na haijalishi shule inazalisha alama ngapi za A. Kupandishwa vyeo walimu wakuu kutazingatia vigezo vingine kama vile wanavyosimamia shule vizuri,'' alisema Ogamba.
Mapema mwaka huu, wizara ya elimu ililazimika kuzuia matokeo ya wanafunzi 4109 walioshukiwa kuhusika na udanganyifu katika mitihani yao ywa mwisho wa mwaka 2023.
Japo idadi kamili ya udanganyifu wa mitihani ipo chini, takwimu zilionyesha kuwa kumekuwa na ongezeko katika miaka ya nyuma.