Wizara ya Afya nchini Kenya imeanzisha Mpango na Maandalizi ya Kitaifa ya Kukabiliana na Mpox, mpango huo unalenga kuongoza hatua za afya ya jamii ili kukomesha mlipuko wa Mpox nchini Kenya na kupunguza hatari ya maambukizi kutoka nje ya nchi.
Nchi jirani zinazokabiliwa na Mpox ni pamoja na Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Burundi na Rwanda.
Serikali ya Kenya inapanga kutumia zaidi ya dola milioni 51.9 kwa jitihada za kukumbana na Mpox.
Hadi sasa Kenya imeripoti maambukizi 5 ya Mpox .
“Mpaka sasa tumechukua vipimo vya wananchi zaidi ya 800,000 na wasafiri katika vituo vyote vya kuingia kwenye maabara zetu za Taifa. Kati ya sampuli 150 tulizochukua kupima, watu143 hawakuambukizwa na Mpox, na wengine 2 tunasubiri matokeo kutoka kwenye maabara, tutaendela kutoa matokeo pale tu tutakapothibitisha iwapo tuna maambukizi mpya au la,” Katibu Mkuu wa Afya ya Umma Mary Muthoni alisema.
Afisa huyo wa wizara ya afya alikuwa katika ziara ya kutathmini kituo cha mpaka cha Llasit huko Loitoktok na kituo cha mpaka cha Namanga katika Kaunti ya Kajiado.
Wizara ya Afya imesema juhudi za udhibiti wa ndani ya nchi zitapokea hadi Ksh.1.7 bilioni ( zaidi ya dola milioni 13.1) ambazo zitatumika miongoni mwa mambo mengine ya ufuatiliaji wa kijamii, kuwapa utaalamu wafanyakazi wa afya, utoaji wa mavazi ya kujikinga, vifaa vya usafi wa mazingira, kuimarisha uchunguzi wa maambukizi na kuweka maeneo ya kutengwa kwa muda.
Kudhibiti kuenea kwa maambukizi ya Mpox katika kanda na katika kaunti zisizozidi tano imetengewa takriban Ksh. 2.3 bilioni ( dola milioni 17.8) na Ksh.941 milioni ( zaidi ya dola milioni 7.2 ) ambayo ni sehemu kubwa ya bajeti yote iliyopangwa kutumika kutoa mafunzo kwa wafanyikazi wa afya.
Harakati za kuvuka mpaka kwenye kaunti zilioko mpakani pia zinachukuliwa kuwa tishio kubwa.