Serikali ya Kenya inasema inataka kuunda sekta ya ndani ya ngozi / Picha: AA

Na Coletta Wanjohi

Bidhaa za ngozi zinafananishwa na watu wenye 'hela nyingi' nchini Kenya.

Pochi cha wanaume cha pesa kinaweza kununuliwa kwa takriban dola 150 wakati kwa mkoba mtu anaweza kutoa zaidi ya dola 300.

"Nchini Kenya, bidhaa za ngozi ni za watu wenye pesa," Camila Njeri anaiambia TRT Afrika," ukiangalia mahali bidhaa hizi zinauzwa, ni wazi kuwa ina wateja wake.

"Sijawahi kuelewa ni kwanini bidhaa za ngozi zinazotengenezwa Kenya hazipatikani kwa wingi ilhali tuna ng'ombe wengi sana katika vijiji vyetu," anaongeza.

Rais William Ruto anapanga kuwekeza zaidi katika sekta ya ngozi nchini na labda kubadilisha hali hii.

"Baada ya miaka miwili nitapiga marufuku uagizaji wa viatu vya ngozi vinavyotengenezwa katika mataifa mengine, ili tuzalishe kwa kutumia ngozi kutoka kwa ng'ombe wetu hapa," Rais William Ruto alisema Jumapili.

"Ngozi zetu wenyewe, tunawapa mbwa kula, na kisha tunaendelea kuagiza bidhaa za ngozi kwa gharama kubwa, karibu dola 200 au hata dola 400," aliongeza, "na bado hakuna kikubwa katika uzalishaji. Ni ngozi sawa na ngozi yetu ng’ombe.”

Rasilimali ya sekta ya ngozi Kenya

Kulingana na ripoti ya 2019 ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Kenya ina zaidi ya ng'ombe milioni 18, mbuzi milioni 27, zaidi ya kondoo milioni 17 na ngamia milioni 3 ambao wanafugwa kwa maziwa na nyama.

Rais Ruto anasema wakulima wengine wanauza ngozi ya mifugo wao kwa chini ya dola moja au kutupa/ Picha others

Ngozi ni baadhi ya bidhaa zinazopatikana wakati mifugo wakichinjwa.

Shirika la Kenya Manufactures Association, linaonyesha kuwa mwaka wa 2019 uagizaji wa ngozi, bidhaa za ngozi, na viatu ulikuwa wa thamani ya zaidi ya $89milioni.

Hii ilikuwa ya juu ikilinganishwa na mauzo ya nje ya hiyo ambayo ilikuwa zaidi ya $70milioni.

Taasisi ya Kenya ya Utafiti na Uchambuzi wa Sera ya Umma inaonyesha "licha ya kuwa nchi ya tano kwa ukubwa wa uzalishaji wa ng'ombe barani Afrika, baada ya Ethiopia, Chad, Sudan, na Tanzania, thamani ya Kenya katika biashara ya ngozi bado ni ndogo."

Rais anasema katika mwaka ujao wa fedha unaoanza tarehe 1 Julai 2023, sekta ya ngozi itapata mgao wa takriban $14milioni.

"Wale wakulima ambao baada ya kuchinja huuza ngozi kwa chini ya dola moja au hata kuzitupa, sasa tutawapangia bei nzuri ya nyama na ngozi," Ruto amesema.

Kufufua sekta ya ngozi

Tedd Josiah, mkurugenzi wa ubunifu katika kampuni ya ngozi ya Jokajok Luxury nchini Kenya, anajikita katika kutengeneza bidhaa mbalimbali za ngozi, huku akiuza Kenya na nchi nyingine za Afrika.

"Viatu, mabegi, na bidhaa nyingine za ngozi zinaweza kutengenezwa ndani ya nchi yetu ili kupunguza uagizaji wa bidhaa hizo na kuleta uwiano wa kibiashara na kutengeneza nafasi za kazi," Josiah anaiambia TRT Afrika.

Anasema kujenga chapa ya Kiafrika kwa bidhaa za ngozi ni muhimu na uamuzi wa serikali kuzingatia kukuza sekta hiyo hata umechelewa.

Tedd Josiah | Picha: Tedd Josiah Twitter

"Haya ni mambo ambayo yanatakiwa kufanywa," Josiah anasema, "ni muhimu kujenga uzalishaji wa thamani, lakini hiyo inamaanisha kujenga majina ya chapa yenye nguvu ya Kiafrika yanayomilikiwa na waafrika ili kuhakikisha urithi kutoka kizazi kimoja hadi kingine."

"Ikiwa mchakato huu utafanywa kwa usahihi ndiyo, inaweza kupunguza bei ya viatu vya shule," Josiah anaongeza, "hata hivyo bado kuna soli za plastiki ambazo zingelazimika kuagizwa kutoka nje, isipokuwa kama baadhi ya viwanda vya plastiki vijiunge katika mchakato huu pia."

Beatrice Mwasa, Mkurugenzi wa Centre for Business Innovation & Training anasema sekta hiyo imechelewa kukua kwa sababu ya kutotekelezwa kwa sera zinazohitajika.

"Soko la ngozi la Kenya ni dola za Marekani milioni 140, na hii ni kidogo ikilinganishwa na thamani ya soko la ngozi la kimataifa ambalo lina thamani ya karibu dola za Marekani bilioni 150." Mwasa anaiambia TRT Afrika.

Anasema changamoto kubwa inayodumaza ukuaji wa sekta hiyo ni kushindwa kwa makampuni ya kati na madogo kushiriki kikamilifu katika uzalishaji kamilifu.

"Sekta hii inatawaliwa na makampuni machache makubwa ya uzalishaji ambayo yanazalisha mapato mengi ya sekta hiyo na yana uwezo wa kudanganya soko," Mwasa anasema.

"kinyume cha hii ni kuwa, biashara nyingi ndogo ndogo zina mchango mdogo kwenye soko. Mpaka sasa, mkazo katika makampuni machache makubwa haujaleta ushindani wa kisekta,” Mwasi ameongezea.

TRT Afrika