Kurugenzi ya upelelezi wa makosa ya jinai DCI nchini Kenya inasema aliyekuwa katibu Mkuu katika Wizara ya Usalama wa Ndani nchini Kenya Dave Munya Mwangi ameshtakiwa kwa ulaghai/ picha DCI

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa katika Wizara ya Usalama wa Ndani nchini Kenya Dave Munya Mwangi ameshtakiwa kwa ulaghai wa ununuzi wa shamba kwa njia ya ulaghai jijini Nairobi.

Kurugenzi ya upelelezi ya makosa ya jinai, DCI nchini Kenya inasema Mwangi alihusika katika kughushi hati ya umiliki akisaidiwa na afisa tapeli katika Wizara ya Ardhi.

Kukamatwa na kufikishwa mahakamani kwa mshtakiwa kulifuatia uchunguzi wa kina wa Wapelelezi wa Ulaghai wa Ardhi, ambao walichunguza malalamiko yaliyowasilishwa na mlalamikaji.

Katika kesi hiyo, washtakiwa kwa pamoja na watu wengine wawili - Sammy Louis Karanja na Moses Ojuka (mfanyakazi wa zamani katika Wizara ya Ardhi na Mipango ya Kimwili) - wanadaiwa kughushi nyaraka za ardhi yenye ukubwa wa hekta 1.591 kwa majina ya kampuni zinazomilikiwa na Mwangi Munya.

Inadaiwa baadaye wakaikodhesha ardhi hiyo kwa kampuni ya Kichina kwa zaidi ya dola 92, 000 ( Shilingi milioni 12).

Baada ya kupekua faili ya kesi hiyo, ofisi ya kiongozi wa mashitaka ODPP ilifanya uamuzi wa kuwashtaki watatu hao kwa makosa matatu ya kula njama, kutoa hati ya uwongo na kughushi hatimiliki.

Dave Munya Mwangi, Mkurugenzi wa Olbolsat Farm Limited alikamatwa na kufikishwa katika Mahakama ya Milimani, ambapo alichukua ombi la kutokuwa na hatia na kuadhibiwa kwa bondi ya zaidi ya dola 154,000 ( shilingi milioni 20) na mbadala wa dhamana ya zaidi ya dola 38,000 ( zaidi ya shilingi milioni 5 ) pesa taslimu.

Wenzake wawili, Sammy Karanja na Moses Ojuka, hawajulikani walipo lakini wanasakwa.

TRT Afrika