Kenya: Jumba la kumbukumbu lakanusha madai kuwa,  nyoka na mamba wamesombwa na maji

Kenya: Jumba la kumbukumbu lakanusha madai kuwa,  nyoka na mamba wamesombwa na maji

Makavazi ya Kitaifa ya Kenya yalisema wanyama walio chini ya uangalizi wake wanasalia na makazi salama, kulingana na taarifa.
Mvua kubwa imesababisha mafuriko katika mji mkuu huku mvua kubwa ikitarajiwa kunyesha. / Picha: Reuters

Mamlaka ya makumbusho nchini Kenya imekanusha madai kuwa wanyama wanaotambaa hatari waliokuwa chini ya ulinzi wake, wakiwemo chatu na mamba, walikuwa wametoroka baada ya kusombwa na maji ya mafuriko ambayo yamesababisha uharibifu mkubwa nchini humo.

Nchi hiyo ya Afrika Mashariki inatatizika kukabili uharibifu wa wiki sita za mvua kubwa na Rais William Ruto alitangaza Ijumaa kuwa taifa hilo linajiandaa kwa kimbunga chake cha kwanza kabisa.

Zaidi ya watu 200 wamekufa tangu Machi huku wengine kadhaa wakipotea, kulingana na data ya serikali.

Makavazi ya Kitaifa ya Kenya yalisema wanyama walio chini ya uangalizi wake wanasalia na makazi salama, kulingana na taarifa.

"Usalama wa maonyesho yetu yote ya moja kwa moja ni muhimu. Kila maonyesho yanahifadhiwa kwa usalama katika eneo lake linalofaa, na kuhakikisha ustawi wao na uhifadhi," ilisema.

Inafuatia madai ambayo hayajathibitishwa kwenye mitandao ya kijamii kwamba wanyama hao watambaao walitoroka kutoka kwa jumba la makumbusho katika mji mkuu, Nairobi.

Kivutio maarufu

Mbuga ya nyoka ya Nairobi iliyo ndani ya jumba la makumbusho la kitaifa la Nairobi ni kivutio maarufu kwa wageni na hutumika kama kituo cha utafiti kuhusu wanyama watambaao na ufugaji wa nyoka.

Hifadhi hiyo pia ni makazi ya wanyama watambaao wenye sumu na wasio na sumu wakiwemo chatu na mamba.

"Hakuna sehemu yoyote ya nchi yetu ambayo imeepushwa na maafa haya," Ruto alisema Ijumaa.

Shule, ambazo zilipaswa kufunguliwa tena Jumatatu, sasa zitasalia kufungwa kwa muda usiojulikana.

TRT Afrika