Rais wa Iran Rais Ebrahim Raisi amefanya mazungumzo na Rais wa Kenya William Ruto jijini Nairobi huku kiongozi huyo wa Iran akianza ziara katika nchi tatu za Afrika.
Majadiliano yao ya Jumatano asubuhi yalilenga zaidi uhusiano wa kiuchumi.
''Kenya ina nia ya kuongeza kiwango cha biashara yake na Iran. Ndio maana tunafanya kazi kwa karibu na Tehran kuwezesha mauzo ya chai zaidi, nyama na bidhaa nyingine za kilimo kwa Iran, ambayo pia itakuwa sehemu muhimu ya kuingia kwa nchi za Asia ya Kati,'' Rais Ruto anasema kwenye mtandao wa Twitter baada ya mkutano huo.
Kando na Kenya, Rais Raisi pia atakwenda Uganda na Zimbabwe. Rais wa Iran Ebrahim Raisi alikuwa amechelewa kuanza ziara ya mataifa matatu barani Afrika ambayo ni ziara ya kwanza ya rais wa nchi hiyo barani Afrika katika kipindi cha miaka 11.
Wizara ya mambo ya nje ya Kenya ilisema ziara hiyo iliyopangwa kuanza Jumanne ilicheleweshwa kwa siku moja ili makubaliano muhimu ya maelewano yakamilishwe.
Ziara ya Rais Raisi inaashiria juhudi za hivi punde zaidi za kidiplomasia za Iran kuunda mashirikiano mapya na kupanua ushawishi wake.