Takriban wakimbizi 500 wanawasili katika kambi hiyo kila siku , hali iliyosababisha uhaba mkubwa wa mahitaji muhimu na kuhatarisha mlipuko wa ugonjwa. Picha :AFP

Watu wawili wamefariki na wengine 1,120 kutibiwa maradhi ya kipindupindu tangu mlipuko wa ugonjwa huo kutokea Novemba mwaka jana.

Mratibu wa Matibabu wa MSF nchini Kenya Dkt. Nitya Udayraj amesema kuwa kambi zilizofurika na ukosefu wa maji safi na imefanya hali kuwa mbaya zaidi. “ Muda wowote tutaona kuzuka janga la maradhi katika kambi kama vile ugonjwa wa homa ya ini.”

Kambi ya Dadaab inajumuisha kambi tatu ndogo, Dagahaley, Ifo na Hagadera ambazo kwa sasa zinawahifadhi zaidi ya wakimbizi 300,000, wengi wao kutoka Somalia, na idadi kubwa wameishi hapo kambini kwa zaidi ya miaka 30.

Mkurugenzi wa MSF nchini Kenya Hassan Maiyaki amesema kuwa, huku zaidi ya watu 500 wakiwasili kila siku, kambi hiyo imefurika kupita kiasi.

“Tayari tumepata mlipuko mbaya wa kipindupindu katika kipindi cha miaka mitano, na kuna hofu ya kutokea magonjwa mengine. Iwapo hili litatokea, litasababisha janga kubwa la kiafya ambayo hatutaweza kumudu kutokana na uhaba wa vifaa na mahitaji muhimu.'' Amesema Bwana Miyaki.

MSF imetoa wito kwa serikali ya Kenya na shirika la wakimbizi UNHCR kuharakisha juhudi za kuwahamisha baadhi ya wakimbizi kwa kambi mpya ya Ifo 2, ambayo imekua ikiandaliwa kwa muda sasa.

TRT Afrika