Maandamano Juni 2021 yalioongozwa na Gen Z yalipinga ongezeko la ushuru na sera za kifedha za serikali ya Rais William Ruto/ Picha: Wengine

Serikali ya Kenya imeanzisha ukaguzi wa deni la taifa la nchi hiyo, kufuatia maandamano makubwa ya kupinga mapendekezo ya ongezeko la ushuru mwezi Juni.

Waziri wa Fedha John Mbadi alithibitisha hatua hiyo kwa shirika la habari la Reuters siku ya Jumatatu, akisema kuwa ukaguzi huo unalenga kufafanua kiasi halisi cha pesa zinazodaiwa na wakopeshaji mbalimbali.

Deni la taifa la Afrika Mashariki kwa sasa linafikia shilingi trilioni 10.5 (dola bilioni 81.71).

Ukaguzi huo ulikuwa miongoni mwa matakwa ya msinigi ya waandamanaji ambao walifanikiwa kuishinikiza serikali kuachana na mipango kadhaa ya nyongeza ya kodi.

Hakuna tarehe ya kutolewa kwa ripoti

Wakati ukaguzi umeanza, Mbadi hakutoa maelezo mahususi kuhusu upeo wa uchunguzi huo au wakati ripoti ya mwisho inatarajiwa.

Mkaguzi mkuu, ofisi huru ya kikatiba inayofadhiliwa na serikali, ndiye anayesimamia mchakato huo.

Awali Rais William Ruto alikuwa ameteua kamati ya kufanya ukaguzi huo, lakini walioteuliwa kadhaa akiwemo mkuu wa Chama cha Wanasheria nchini Kenya walikataa jukumu hilo wakisisitiza kuwa jukumu hilo likabidhiwe mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali.

Wakati alipokua anaulizwa maswali bungeni baada ya kuteuliwa na raisi kuwa waziri wa fedha, Mbadi aliahidi kuimarisha "uwajibikaji wa madeni" na kukuza uelewa wa umma wa hali ya kifedha ya nchi.

Maandamano hayo, ambayo yalisababisha vifo vya zaidi ya watu 50, yalimlazimu Rais Ruto kuachana na sheria ya ufadhili wa serikali na kusababisha kupungua kwa viwango vya mikopo kutoka kwa mashirika makubwa ya viwango vya kimataifa.

Wakati huo huo, timu kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa kwa sasa iko nchini Kenya kwa kazi ya kutafuta ukweli. Bodi ya IMF imeratibiwa kukutana ili kukagua mpango wa kiuchumi wa Kenya na uwezekano wa kuidhinisha ugawaji wa dola milioni 600.

TRT Afrika