Kenya imejiunga na Taasisi ya Kimataifa ya Chanjo, International Vaccine Institute(IVI).
IVI ni shirika la kimataifa lenye dhamira ya kugundua, kuendeleza, na kutoa chanjo salama, bora na nafuu kwa afya ya kimataifa kwa nchi mwanachama kwa lengo la kukuza uzalishaji wa chanjo nchini.
"Kuongezeka kwa upatikanaji wa chanjo kutaimarisha utoaji wa huduma zetu za msingi za afya na kuzuia magonjwa," Rais wa Kenya William Ruto amesema katika akaunti yake ya X.
IVI imejitolea kuanzisha Ofisi ya nchi na Mradi jijini Nairobi, kwa ajili ya utendajikazi wa Kuendeleza Chanjo (AVEC).
"Kenya itafaidika na utaalamu wa kimataifa wa IVI na uwezo wa utengenezaji wa dawa, ikiwa ni pamoja na uhamisho wa teknolojia kwa kutengeneza chanjo kama zile za kipindupindu, surua, rubela na typhoid," Waiziri wa Afya Nakhumicha Wafula amesema katika makubaliano yaliyofanywa katika ziara ya rais huko Korea.
"Kenya itafaidika kutokana na uwekezaji wa kigeni wa moja kwa moja katika majaribio ya kimatibabu ya chanjo, na miradi 2 ya chanjo hadi dola milioni 50 itakayoandaliwa katika BioVax na mamlaka ya utafiti wa matibabu, KEMRI. Ushirikiano huu utaunda fursa za ajira na kutoa mafunzo ya kina kwa wataalamu wa Kenya katika utengenezaji wa chanjo,” ameongeza kusema Waziri huyo.
Taasisi ya Kimataifa ya Chanjo, International Vaccine Institute(IVI) ni nini?
Taasisi ya Kimataifa ya Chanjo, IVI, ni Shirika la Kimataifa lililoanzishwa mwaka 1997 kama mpango wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).
Bangladesh, Brazili, China, Ekuador, Ufini, India, Liberia, Mongolia, Uholanzi, Oman, Pakistan, Panama, Peru, Ufilipino, Jamhuri ya Korea, Rwanda, Uhispania, Sri Lanka, Uswidi, Thailand, Falme za Kiarabu, Uzbekistan, Vietnam, na Shirika la Afya Duniani, WHO ni wanachama wa mkataba wa uanzishaji wa IVI.
Ni miongoni mwa mashirika machache duniani yanayoangazia upatikanaji wa chanjo.
IVI inaangazia chanjo dhidi ya magonjwa ya kuambukiza na kuhakikisha chanjo zinapatikana kwa idadi ya watu walio hatarini katika nchi zinazoendelea.
Ina makao makuu Seoul nchini Korea na barani Afrika ina vituo vya ushirikiano nchini Ghana, Ethiopia, na Madagascar.
Shirika hili lina maabara sita na kukuza ushirikiano endelevu na serikali, taasisi za kitaaluma, sekta, uhisani na mashirika mengine ya afya duniani.