Kenya imesema kuwa iko tayari kuchangia kikosi cha kimataifa cha kusaidia Haiti kurejesha 'nidhamu na utulivu.'
Katika taarifa iliyochapisha katika mtandao wa Twitter, waziri wa mambo ya nje Alfred Mutua amesema kuwa hii ni katika kujibu ombi la Haiti kwa jamii ya Kimataifa.
''Ahadi ya Kenya ni kupeleka kikosi cha polisi 1,000 kusaidia kutoa mafunzo na kusaidia polisi wa Haiti kurejesha hali ya kawaida nchini na kulinda mitambo ya kimkakati.'' Taarifa hiyo ilisema.
Makundi ya wahalifu yanadhibiti takriban 80% ya mji mkuu wa Haiti, na uhalifu wa kikatili kama vile utekaji nyara kwa ajili ya fidia, wizi wa kutumia silaha na utekaji nyara wa magari ni miongoni mwa uhalifu unaodaiwa kuwashinda nguvu polisi wa Haiti.
Kwa takriban mwaka mmoja, Haiti, kupitia Umoja wa Mataifa imekuwa ikiomba uingiliaji kati wa kimataifa kusaidia polisi wake, lakini hakuna nchi yoyote iliyojitokeza kufikia sasa.
Idhini kamili kutolewa
Haijabainika nchi ganinyingine itakayo jiunga na Kenya katika oparesheni hii, au iwapo Kenya itarusiwa kuendelea kivyake, ila imesema kuwa iko tayari wakati wowote wakipewa idhini.
''Mpango huo bado unasubiri mamlaka kutoka kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na idhini kutoka kwa mamlaka ya ndani,'' alisema Mutua katika taarifa yake.