Naibu Rais wa Kenya Rigathi Gachagua akifika bungeni kabla ya Bunge la Seneti kuchunguza hoja ya kumuondoa madarakani/ Picha:  Seneti ya Kenya 

Bunge la Seneti nchini kenya limeanza majadiliano ya siku mbili ya kuchunguza hoja wa kuondolewa madarakani kwa Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Naibu Rais kuwa amesema kupitia mawakili wake hana hatia ya kumdhoofisha Rais, Baraza la Mawaziri na utekelezaji wa mamlaka ya serikali kwa madai ya kutoa matamshi kwa umma ya upande mmoja ambayo hayakuendana na misimamo ya sera iliyopitishwa kwa pamoja na serikali.

Spika wa Seneti Amason Kingi ametupilia mbali pingamizi la mawakili wa Naibu Rais Rigathi Gachagua lililotaka kumzuia Gavana wa Siaya James Orengo kuwakilisha katika Bunge la Kitaifa wakati wa kusikizwa kwa hoja yake ya kuondolewa madarakani.

Mawakili wa Gachagua wamepinga uamuzi wa kuwepo kwa mashahidi ambao hawajulikani.

"Hakuna kitakachokuwa cha upendeleo zaidi ya kuwaita mashahidi ambao hatujaona maelezo au viapo. Kama hii inaruhusiwa kwa Bunge la Kitaifa kuita mashahidi bila kutoa maelezo ya awali, basi kesi itakuwa na upendeleo kwa hivyo tunapinga hilo," Paul Muite kiongozi wa kikundi cha mawakili wanaomuakilisha Naibu Rais Rigathi Gachagua amekiambia kikao cha seneti.

"Mbali na kuheshimu sheri za bunge hili la seneti, katiba yetu lazima ipewe heshima. Kitengo cha 50 ambacho kinampa mtu haki ya kesi mahakamani," Muite ameongezea.

"Hakuna maelezo kamili ya kwa nini Tume ya Kukumbana na Ufisadi haikuulizwa ifanye uchunguzi wa madai kabla madai hayo kufikishwa mbele ya Bunge la Taifa kabla ya uamuzi kufanyika kwa sababu Bunge la Taifa halina uwezo wa kuchunguza makosa ya jinai," aliongezea.

Gavana wa Siaya James Orengo ambaye sasa anawakilisha Bunge la Taifa kama wakili wake, amesema kuwa Bunge la Seneti sio geni katika mchakato wa kumuondoa mtu kwa nguvu madarakani chini ya katiba. Akitoa mifano ya kesi za kuondolewa kwa magavana na naibu magavana kupitia seneti.

"Ushahidi unaonyesha kuwa Naibu Rais alikuwa akivamia pesa ambazo kweli zilikuwa mali ya marehemu kaka yake ili kupata mali. Haya yalikuwa mapato ya uhalifu uliofanywa na DP ili kupata mali," Orengo alidai.

Amedai kuwa Gachagua alienda katika hospitali London, Uingereza mwaka 2017 ambapo ndugu yake alikuwa amelazwa na akamlazimisha kaka yake amuandike katika wosia wake ili apate mali. Lakini hoja ilipingwa vikali na wakili Elisha Ongoya ambaye alisema kuwa Naibu Rais anafaa kuheshimiwa.

Pia amemtuhumu Naibu Rais kwa madai kuwa alichaguliwa ili kufuatilia maslahi ya watu wa kabila lake.

Naibu Rais anashutumiwa kwa kutamka maneno yanayoashiria kuwa kutaka kupewa hisa za watu wa kabila lake.

"Kuzungumza kuhusu wanahisa na baadhi ya watu kuweza kuvuna kwa misingi ya umiliki wa hisa ni jambo la kuchukiza na linakinzana na vifungu vya katiba yetu," Orengo alisema.

Wakili Elisha Ongoya naye alidai kuwa hoja ya kutaka kumuondoa Naibu Rais haifai.

"Hoja ya kutaka kumuondoa Naibu Rais iliyowasilishwa na kuidhinishwa na Bunge itasalia katika historia yetu ya kikatiba ikiwa ni hoja ya aibu kuwahi kupitishwa na bunge katika Jumuiya ya Madola," aliambia Seneti.

"Je, kuna ushahidi wa kuaminika wa makosa ya ajabu ya Gachagua, na kuna uthibitisho wa kutosha wa tuhuma dhidi yake?" aliuliza.

Wakili wa bunge pia amemkashifu Naibu Rais kwa kujadili masuala ya kiusalama hadharani ilhali yeye ndiye wa pili kwa uongozi wa nchi.

Bunge la Seneti litaendelea kuchunguza kesi ya Gachagua 17 Oktoba 2024 ambapo naye pia atapewa muda wa saa 4 kujitetetea mbele ya maseneta.

TRT Afrika