Na Charles Mgbolu
Ni usiku wa manane, lakini kundi la wasanii wa Tanzania wapo katika studio zao jijini Dar es Salaam wakipekua michoro na picha za rangi huku wakiunda makatuni katika kompyuta zao, zinazoangazia mada ngumu kwa njia ya kueleweka kwa urahisi na vijana.
Mradi huu unatumia Sanaa katika kuleta mabadiliko katika jamii juu ya mada zinazotazamiwa kuwa mwiko kuzungumzia kama vile afya ya akili au ngumu kueleweka, miongoni mwa wanafunzi wa shule.
"Kama kikosi cha mradi huu, tulikuwa tunazuru mashule, kuwaelimisha na kuwahamasisha wanafunzi wakae shuleni, na kuzingatia masomo yao," Ian Tarimo, 35, ameambia TRT Afrika.
Tarimo alianza kwa kuandaa warsha mashuleni miaka kumi iliyopita pamoja na marafiki zake, Gwamaka Mwabuka na Alphonce Haule, lakini baadaye wakaamua kuanzisha mradi huu wa kutengeneza katuni miaka saba iliypita.
Kundi lao la utengenezaji vibonzo linalojiita Tai Tanzania linatumia mfumo wa katuni za 3D, tamthilia za redio na vichekesho, kutoa mafunzo na kujaribu kuziba pengo linaloachwa kutokana na idadi kubwa ya watoto wasiohudhuria shule Tanzania.
Ni wazo zuri kutokana na kuwa idadi ya watoto wasiokwenda shule Tanzania ni kubwa na ya kusikitisha. Takwimu zinaonesha idadi hiyo kuwa zaidi ya watoto milioni 1.8 kati ya miaka 7 -13, kwa mujibu wa ripoti ya Benki ya Dunia ya 2020.
Takriban 70% ya watoto kati ya miaka 14–17 hawajasajiliwa elimu ya sekondari ilihali 3.2% pekee ndio waliosajiliwa miaka miwili ya mwisho ya shule.
UNICEF inasema kuwa kijumla watoto kutoka familia za pato la chini waliofika umri wa kwenda shule ndio walio na uwezekano mkubwa zaidi kukosa shule.
"Nilitaka kuchangia katika kupunguza idadi hiyo. Ukawa mradi wa kibinafsi kutaka kuwasaidia watu kuishi maisha bora kupitia elimu bora na wasiwe wanaponzwa kwa kukosa elimu maishani,” ameambia TRTA Afrika.
Athari kubwa
Lakini Tarimo alipata ugumu kufanikisha wazo hili kutokana na kushindwa kwa wanafunzi kuvumilia na kufuatilia warsha zake.
"Nilitambua punde tu kuwa wanafunzi hao walijiondoa, na baada ya kumalizika darasa pengine asili mia 20 pekee walikuwa bado wananisikiliza.’’
Hapo ndipo aliamua kutumia ubunifu kuwavutia wanafunzi.
"Tuliamua kama kikundi kufuata mkondo huu wa kutumia katuni kwani tuliona ndio njia bora zaidi ya kupitisha ujumbe kutokana na uwezo wake mkubwa kunasa akili za watoto na kusisimua ubongo," amesema.
Iliwachukua miezi sita, muda mrefu zaidi ya walivyotarajia kuandaa filamu ya kwanza ya dakika tatu. Mwezi Oktoba 2017 filamu yake ya kwanza hatimaye ilizinduliwa.
''Tulikuwa na mtu mmoja tu aliyekuwa na uzoefu wa kubuni katuni na mwelekezi mmoja wa filamu... Tukaanza kuwatumia watu wa kujitolea hapa ofisini kuzipa sauti katuni hizo. Hata mimi nakumbuka nilikuwa sauti ya baba wakati mmoja.
Changamoto kubwa zaidi ilikuwa kurahisisha mada nzito kueleweka zaidi na watoto.
"Tulipotunga katuni juu ya malaria, tuliamua kupatia ugonjwa huo umbile lenye sura na sauti na kuelezea hadithi ya kuvutia juu ya mwili wa binadamu ulivyovamiwa na jeshi la mbu," aliongeza.
Darasa linajaa
Katuni hizi zilijumuisha wahusika wa asili ya kiafrika waliozungumza lugha ya Kiswahili – ambayo ndio lugha inayozungumzwa kote Tanzania. Na hapo hapo filamu hizo zikapata umaarufu mkubwa.
Tarimo na kundi lake wanagusia pia mada za afya ambazo kwa kawaida zinaonekana kuwa mwiko kuzungumzia katika jamii.
Anasema kuwa hii inasaidia wanafunzi wake kuelewa zaidi magonjwa na njia za kujiepusha na maambukizi na pia njia bora za kuimarisha afya zao.
"Mama yangu alikuwa muuguzi na baba alikuwa mwalimu. Kwa hiyo naona kama nilijaaliwa kutoa mafunzo juu ya masuala ya afya.’’ Anasema Tarimo.
“Kama tutaweza kuzungumzia wazi mtu kupata homa, ambacho ni kitu cha kawaida kibayojia, kwanini basi tuone haya kuzungumzia suala la afya ya akili au afya ya uzazi. Hazifai kuwa mwiko,’’ alisema.
"Darasa letu lilijaa kila mara. Kila mmoja, licha ya umri wake, alivutiwa sana.'' alielezea.
Kutambuliwa kimataifa
"Tatika hadithi zetu, nilitaka ziwe asili za kiafrika, zinazotutambulisha na tunaweza kujivunia,'' alisema.
Filamu hiyo ya katuni imepokea tuzo mbali mbali ikiwemo tuzo bora zaidi ya katuni katika tamasha la 2021 la filamu Tanzania na tuzo ya filamu bora zaidi ya katuni Afrika Mashariki, katika tamasha la kimataifa la Kwetu 2022.
Kundi hilo pia limeshirikiana na mashirika ya kimataifa chini ya Umoja wa Mataifa yakiwemo UNICEF, UNESCO, na UNFPA.
Katuni za Tai Tanzania zinawafikia zaidi ya watu milioni 12 katika mitandao ya kijamii na zinapata zaidi ya watazamaji milioni 4 kupitia televisheni washirika. Watazamaji wao wanatapakaa ndani na nje ya bara Afrika.
"Inatia moyo sana ukiona kazi unayofanya kwa nia safi ikipokewa vyema na wengi. Hili linanisukuma kujitolea zaidi. Ni kitu cha kuridhisha mno," anasema Tarimo.