Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara wa Uganda Geraldine Ssali Busulwa amekamatwa kwa madai ya ufisadi/ Picha: Wengine photo

Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara, Viwanda na Ushirika, Geraldine Ssali Busulwa, alilala katika Kituo cha Polisi cha Tarafa ya Kira.

Siku ya Ijumaa, aliratibiwa kufika mbele ya Mahakama ya Kupambana na Ufisadi kwa mashtaka yanayohusiana na kuelekeza pesa zilizokusudiwa na serikali kuwafidia waathiriwa wa vita kupitia SACCOs zao za ushirika.

Ssali alikamatwa Ijumaa na kufikishwa katika Mahakama ya Kupambana na Rushwa baada ya kuhojiwa na polisi.

Hata hivyo, Hakimu Joan Aciro alikataa kusomwa kwa mashtaka hayo na badala yake alimrudisha kwa polisi, akisubiri uamuzi wa uhalali wa hati ya mashtaka iliyofanyiwa marekebisho iliyowasilishwa na Mkurugenzi wa Mashtaka.

Mwendesha Mashtaka alisema Geraldine Ssali Busulwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/2022 na 2022/2023 akiwa Katibu Mkuu na kukabidhiwa nafasi ya Afisa Masuuli katika Wizara ya Biashara, Viwanda na Ushirika, aliweka kampuni ya Buyaka Growers kati ya zile zitakazolipwa kwa athari za vita.

Hata hivyo, hii haikuwa imeorodheshwa katika bajeti ya ziada ya Agosti 2021.

Pia inadaiwa kuwa Ssali katika kutekeleza majukumu yake zaidi, alilipa malipo yasiyo ya kawaida ya shilingi bilioni 3. 8 ( Dola milioni 1) kwa Kirya na mawakili wa kampuni.

Anadaiwa kuwa alifanya malipo haya kupitia Julius Kirya Taitankonko kwa madai ya kuwalipa fidia waathirika wa vita wa ushirika wa Buyaka Growers, akijua vyema kwamba hatua zake zitaisababishia serikali hasara ya kifedha kwa sababu malipo hayo yalikiuka maagizo ya Hazina ya 2017.

Kukamatwa kwake kunakuja huku Rais Yoweri Museveni akitangaza vita vikali dhidi ya ufisadi.

TRT Afrika