Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limelaani vikali ongezeko la vitendo vya utekaji na mauaji ya watu unaoendelea nchini humo.
Akisoma ujumbe wa TEC siku ya Septemba 15, 2024 wakati wa kelele cha Kilele cha Kongamano la 5 la Ekaristi Takatifu Kitaifa katika Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam Makamu Rais wa TEC, Askofu Eusebius Nzigilwa alioneshwa kusikitishwa na ongezeko la vitendo vya namna hiyo.
“Matukio ya namna hii yanatuacha na maswali mengi, ni wapi taifa letu linaelekea. Ni kweli kuwa mamlaka zetu zimezidiwa na kiasi kwamba wanashindwa kudhibiti mwenendo huu?” alihoji Askofu Nzigilwa.
Askofu huyo pia alisisitiza kuwa ni lazima vikundi vya kihalifu vidhibitiwe ili visivizidi nguvu vyombo vya dola.
Amevitaka vyombo vya dola na taasisi zingine nchini Tanzania kutimiza wajibu wao katika kurejesha amani na utulivu nchini humo.
“Hatuamini kuwa vikundi vya kihalifu vina nguvu kuliko vyombo vyetu vya dola. Kwahiyo, tunatoa rai kwao kuchukua hatua madhubuti kulinda tunu za taifa letu ili tuishi kwa amani,” alisema.
Kulingana na Askofu Nzigilwa, uhai ni zawadi kutoka kwa Mungu na kwamba utu na maisha ni lazima viheshimiwe na kulindwa kwa gharama yoyote ile.
Mapema Septemba 6, Katibu Mkuu wa CHADEMA John Mnyika, alitangaza tukio la kutekwa kwa Mjumbe wa Sekretarieti ya Taifa ya chama hicho, Ally Mohamed Kibao.
Siku mbili baadaye, mwili wa Kibao ulipatikana katika eneo la Ununio jijini Dar es Salaam ukiwa na majeraha sehemu mbalimbali na kwenda kuhifadhiwa kwenye hospitali ya rufaa ya Mwananyamala, kabla haujatambuliwa na ndugu zake, wakiwemo pia viongozi wa CHADEMA, waliokuwa wanaongozwa na mwenyekiti wao Freeman Mbowe.