Kamanda wa kikosi cha Jumuiya ya Afrika Mashariki, Aphaxard Kiugu./Picha: TRTAfrika

Majeshi ya kulinda amani kutoka Jumuiya ya Kusini mwa Afrika (SADC) yameingia Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, tayari kwa jukumu la kurejesha amani eneo hilo.

Vikosi vya SADC vinachukua nafasi ya majeshi ya kulinda amani kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACRF) ambayo yamemaliza muda wake.

Akizungumza mara baada ya kupokea bendera kutoka kwa Kamanda wa EACRF Aphaxard Kiugu, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Peter Mathuki amesisitiza kuwa EAC itaendelea kuimarisha uwezo wake wa kukabiliana na changamoto za amani na usalama katika nchi wanachama ikiwa ni pamoja na kuunda sera, miongozo, mifumo na vyombo vinavyozingatia kanuni bora za kimataifa.

" Uwepo wa majeshi yetu Mashariki ya DRC unathibitisha uwezo wetu katika kukabiliana na changamoto za usalama na pia kama mshirika muhimu katika kutafuta suluhu ya matatizo ya kikanda," Mathuki anasema.

Katibu Mkuu huyo, pia aliupongeza uhodari, ushupavu na ujasiri uliooneshwa na EACRF wakati wote wa kulinda amani katika eneo hilo, akisema kazi hiyo ilikuwa ni ya mafanikio pamoja na changamoto zilizojitokeza.

Jukumu la EACRF nchini Congo lilitamatika Disemba 21, 2023 huku vikosi vya SADC vikiingia Mashariki ya Congo hivi karibuni.

Kikosi hicho kiliundwa na wanajeshi kutoka Kenya, Uganda, Burundi na Sudan Kusini, na kutumwa mashariki mwa DRC mwishoni mwa mwaka 2022, kusaidia kuleta amani.

Hata hivyo, Serikali ya nchi hiyo ilivishutumu vikosi hivyo kwa kushindwa kuwakabili waasi wa M23.

Baadhi ya Majeshi ya Kulinda amani Mashariki mwa Congo yakiwa katika doria./Picha: Wengine

Kwa upande wake, mkuu wa vikosi vya EACRF Meja Jenerali Kiugu anasema vikosi vyake vimefanikiwa kuwalinda raia wa eneo hilo, kubwa ikiwa ni kuwezesha kuwepo kwa makubaliano ya kumaliza vita kati ya Majeshi ya Ulinzi ya DRC (FARDC) na M23.

TRT Afrika