Na Kevin Philips Momanyi
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki
Hatimaye, Mahakama Kuu ya nchini Kenya imempa Joseph Irungu maarufu kama Jowie, adhabu ya kifo kufuatia mauaji ya mfanyabiashara Monica Kimani, Septemba 2018.
Mwili wa Monica ulipatikana bafuni ukiwa na majeraha makubwa mwilini mwake huku miguu yake ikiwa imefungwa nyaya.
Kabla ya kifo chake, Monica alikuwa anasimamia biashara za familia yao huko Juba, Sudan ya Kusini.
Mahakama ya nchi hiyo ilibaini kuwa Jowie alitumia kitambulisho kilichoghushiwa kuingia katika nyumba ya Monica.
Mahakama pia iligundua kuwa Jowie alitumia bunduki aliyoazima kutoka kwa Brian Kasaine, rafiki yake wa karibu kabla ya kutekeleza mauaji hayo, ingawa alidai kuwa hakuwa anamfahamu Monica.
Jowie aliteketeza nguo zake kwa moto, katika jitihada za kuficha ushahidi wa kitendo chake.
Hata hivyo, miaka sita baadae, sababu ya Jowie kumuua aliyekuwa mpenzi wake bado hazijajulikana.
Joseph Irungu, mtaalamu wa masuala ya usalama, alizaliwa Nakuru Novemba 20, 1990.
Alikutana na Monica mara baada ya kumaliza kusomea stashahada katika uzalishaji wa Chakula katika chuo cha Kenya Polytechnic mwaka 2011.
Baadaye alihamia Dubai ambako alifanya kazi katika kampuni ya ulinzi mara baada ya kupokea mafunzo ya mbinu za ulinzi wa kijeshi kutoka Chuo cha Polisi cha Dubai cha Ogara Group.
Jowie alipata leseni ya kutoa huduma za ulinzi binafsi kwa wanasiasa.
Katika shitaka hilo, Jowie aliunganishwa na mtangazaji maarufu Jacque Maribe, kabla ya Mahakama hiyo hiyo kumuondolea kuondolewa kwa mashitaka dhidi yake.
Wakati Jowie anajiandaa na maisha mapya jela, serikali ya Kenya, hivi karibuni ilimuajiri Maribe kama Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano katika Wizara ya Utumishi wa Umma.
Kifo ni adhabu ya kabisa katika sheria za Kenya. Hata hivyo, nchi hiyo haijawahi kutekeleza hukumu hiyo tangu mwaka 1987.