Jiji la Rabat linakuwa la tano barani Afrika kupata sifa ya 'Makao Makuu ya Vitabu', ikitanguliwa na Alexandria, Port Harcourt, Conakry na Accra./Picha: Getty

Na Sylvia Chebet

TRT Afrika, Istanbul, Uturuki

Kama tu zilivyo makumbusho mbalimbali, majiji makubwa ulimwenguni huakisi utajiri wa kihistoria, mila na tamaduni.

Mji wa mkuu wa Morocco, Rabat ni kiashirio tosha cha kile kinachotafutwa na waandishi wa riwaya, kama vile mitaa, vichochoro, majengo na sehemu za wazi.

Kama mwandishi wa Morocco Tahar Ben Jelloun anavyosema, "Rabat ni mahali ambapo mapokeo yanakutana na usasa, huku fasihi ni daraja kati ya vitu hivyo viwili."

Kauli ya Jelloun inahalalishwa na maamuzi ya Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO, Audrey Azoulay ya mwezi huu, alipotangaza kwamba Rabat imeteuliwa kuwa "Mji Mkuu wa Vitabu vya Dunia 2026".

Jiji la Rabat linakuwa la 26 duniani kupata hadhi hiyo toka mwaka 2001, likipokea kijiti kutoka kwa mji mkuu wa Brazil, Rio de Janeiro.

Ni mji pekee wa tano barani Afrika kupata hadhi hiyo baada ya Alexandria nchini Misri (2002), Port Harcourt nchini Nigeria (2014) mji mkuu wa Guinea, Conakry (2017) and Accra nchini Ghana mwaka 2023.

"Kutangazwa kama mjii mkuu wa vitabu ulimwenguni ni sifa kubwa sana kwa jumuiya ya fasihi ya Rabat," Mkurugenzi wa vitabu, maktaba na kumbukumbu za kale, Latifa Moftaqir, anaiambia TRT Afrika.

"Heshima hii kubwa inaliweka jiji la Rabat kwenye ramani ya ulimwengu. Ni ishara kuwa bara la Afrika linazidi kupata umaarufu kutokana na mchango wa fasihi yake."

Kamati ya ushauri ya UNESCO ilizingatia vigezo vya utajiri wa kitamaduni na utayari wa kutunza urithi wa utamaduni, wakati wa kutoa maamuzi hayo.

Mseto wa mambo ya kale na mambo mapya

Waandishi na washairi mbalimbali wameuelezea mji wa Rabat kama kitovu cha utamaduni na fasihi./Picha: Reuters

Rais wa zamani wa Umoja wa Waandishi wa vitabu wa Morocco, Hassan Najmi anauelezea Rabat kama "mji wa mwanga".

"Ni mji msafi na wa kupendeza ukiwa na vyuo vikuu vingi na wasomi wengi," anaimabia TRT Afrika. Ukiwa umeanzishwa kwenye karne ya 12, mji wa Rabat unapatikana katika bahari ya Atlantiki kaskazini magharibi mwa Morocco.

Mseto wa mambo ya kale na mambo mapya ukisherehekewa kwenye sanaa ya ushairi nchini Morocco, na kuzaa kitu kinachoitwa "makao makuu ya utamaduni, fasihi na ubinifu", kulingana na Najmi.

"Rabat ni njia panda ya utamaduni ambapo vitabu husambaza maarifa na sanaa katika utofauti wake.

Ukuwaji wa sekta ya vitabu na usomaji ni jitahada nzuri ya kukuza elimu," anasema Azoulay, akiongeza: "Haya yanaakisi malengo ya UNESCO."

Wazo la "mji mkuu wa vitabu" limeanzia kwenye katiba ya UNESCO mwaka 1945: "Kwa kuwa vita huanzia kwenye fikra za wanaume, ni fikra hizo hizo zinapaswa kuwa ulinzi wa amani."

Ikiwa na viwanda 54 vya uchapishaji, maonesho ya tatu ya kimataifa ya vitabu na uchapishaji barani Afrika na idadi inayoongezeka ya maduka ya vitabu, UNESCO inabainisha kuwa tasnia ya vitabu ya Rabat iko mstari wa mbele katika kuleta maarifa ya kidemokrasia.

UNESCO, kupitia kamati yake ya ushauri, iliitambua dhamira ya wazi ya Rabat ya kuendeleza fasihi, wanawake, na vijana kupitia kusoma na mapambano dhidi ya kutojua kusoma na kuandika", haswa miongoni mwa jamii ambazo hazijahudumiwa.

Kuendeleza utamaduni wa kusoma

Ukuaji wa sekta ya vitabu jijini Rabat unakuza elimu./Picha: AFP

Kulingana na Moftaqir, utamaduni wa usomaji wa nchini Morocco ni wa "wastani", ingawa unabadilika polepole, haswa miongoni mwa kizazi kipya. "Vyuo vikuu, programu za kusoma na kuandika, na maktaba za umma zimekuwa na jukumu katika kukuza usomaji.

Uwepo wa migahawa ya fasihi na maonesho ya vitabu pia yamechangia ukuaji wa utamaduni thabiti wa kusoma," anaiambia TRT Afrika.

Jiji lolote lililoteuliwa kuwa Mji Mkuu wa Vitabu vya Ulimwenguni wa UNESCO unatakiwa kutangaza vitabu na usomaji kwa kila kizazi na makundi, ndani na nje ya mipaka ya kitaifa, na kuandaa mfululizo wa shughuli za fasihi mwaka mzima.

Mwezi Aprili 2026, Rabat itakuwa mwanzo wa mpango wa kuimarisha ujuzi wa kusoma na kuandika miongoni mwa Wamorocco kupitia sherehe ya mwaka mzima.

"Ni muhimu kuleta pamoja nguvu zinazoendesha eneo la kitamaduni na fasihi la Morocco - waandishi, washairi, wasomi na wachapishaji - ili kuunda wakati mzuri katika 2026," anasema mshairi na mtunzi wa riwaya Najmi.

Yeye na Jelloun tayari wanahesabiwa kuwa miongoni mwa wataalamu bora zaidi wa fasihi duniani. Majina mengine mashuhuri kwenye orodha hiyo ni pamoja na Abdelfettah Kilito, maarufu kwa insha na uhakiki wake wa kifasihi na Abdellatif Laabi, mshairi na mwanahabari.

Orodha ya miji mikuu ya vitabu ulimwenguni
TRT Afrika