Jeshi la Polisi nchini Tanzania limetoa wito kwa yeyote mwenye taarifa kuhusiana na kifo cha aliyekuwa Mjumbe wa Sekretarieti ya CHADEMA Ally Mohamed Kibao, aziwasilishe ili kusaidia kufanikisha kukamilika mapema kwa tukio hilo.
"Timu ya uchunguzi wa matukio makubwa toka Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai toka Makao Makuu imetumwa kuongeza nguvu ili kuhakikisha waliofanya mauaji wanakamatwa na kufikishwa mahakamani," ilisema taarifa hiyo iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini Tanzania, David Misime.
Mwili wa Kibao ulipatikana katika eneo la Ununio jijini Dar es Salaam ukiwa na majeraha sehemu mbalimbali na kwenda kuhifadhiwa kwenye hospitali ya rufaa ya Mwananyamala, kabla haujatambuliwa na ndugu zake, wakiwemo pia viongozi wa CHADEMA, waliokuwa wanaongozwa na mwenyekiti wao Freeman Mbowe, siku ya Septemba 8, 2024.
Mwanachama huyo wa CHADEMA aliripotiwa 'kutekwa' na watu wasiojulikana akiwa ndani ya basi siku ya Septemba 6.