Na Lulu Sanga
Siku moja iliyopita, waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) nchini Tanzania Dkt. Selemani Jafo alisema Serikali inazihimiza taasisi binafsi na za uma kwa sasa kutumia nishati mbadala ambayo ni safi kwa ajili ya kupikia.
Waziri huyo wa Tanzania amesema watumiaji wakubwa wa nishati za kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia ni taasisi za umma na binafsi, hivyo kutokana na athari zake kimazingira, kiafya, kijamii na kiuchumi, serikali ya nchi hiyo imeandaa Dira ya Taifa
Dira hiyo itahusisha matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia pamoja na Mpango Mkakati wa Utekelezaji wa Dira hiyo kwa kipindi cha miaka kumi hadi kufikia 2033.
Lakini je mpango huu unatekelezeka?
Mpango huu unaousisha taasisi za uma na binafsi kote mijini na vijijini huenda ukawa na uhalisia.
Mama Rose mmiliki wa kampuni ya upishi Tanzania anasema naona kama wanaharakisha sana lakini gesi na umeme pekeake ni ngumu.
"Mkaa bwana unanafasi yake kubwa kwenye kupika wali na pilau niwaambie tu twende taratibu" anamaliza mwanamke huyo anayejishughulisha na biashara ya upishi.
TRT Afrika imezungumza na Jacquiline Masawe Mratibu wa miradi ya ustahimilivu na mabadiliko ya tabia ya nchi anasema uwezekano upo ila muda uliotengwa ni mdogo.
"Uwezekano wa kutekelezeka upo lakini kwa muda uliowekwa ni ngumu kutekelezeka kwa uhalisia. Kwasasa sera za nchi bado inaruhusu utumiaji wa nishati mchanganyiko" anasema Jaquiline kutoka Climate Action network Tanzania
Hata hivyo mtaalamu huyo ameainisha kuwa kuna mambo mengi ambayo yanaweza kuwa kikwazo katika kutekeleza mpango huo kabambe unaolenga kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi Tanzania.
"Matumizi ya mkaa na kuni yanahusisha kipato cha moja kwa moja hivyo kwa sasa bado kwa mtanzania wa vijijini au taasisi changa hawawezi kumudu gharama za gesi au umeme" anasema Jaquline
Vilevile amefafanua kuwa imani, tabia na tamaduni za kitanzania pia bado ni changamoto kwasababu kuna watu wanaamini ladha ya chakula inaongezwa na nishati unayo tumia.
"Kuna mtu bado anaamini utamu wa ubwabwa ni kupika kwenye mkaa, mwingine ugali ili uive ni kupika kwa kuni. Lakini pia kuna hofu kuwa gesi na umeme ni hatari kwa nyumba yaani si salama, hii yote inafanya kutimia kwa malengo yaliyotangaza inakuwa ni ngumu"
Je nini kifanayike ili kufikia lengo tajwa la serikali?
Kwa mujibu wa mtaalamu huyo wa mazingira Bado unahitajika ushirikiano mkubwa baina ya serikali na wadau kuelimisha na kuboresha sera na mipango yake na kujenga upya mazingira rahisi ya kupatikana kwa nishati salama kwa gharama nafuu.
"Serikali itapaswa kuhakikisha taarifa hii inawafikia raia wote kwa wakati ili waanze kujenga mazoea taratibu ya kuacha kutumia kuni na mkaa"
Hata hivyo anaongeza kuwa elimu kubwa inahitajika kwa wafanyakazi wa serikali na taasisi ambao ndio wanapaswa kuanza kufanya utekelezaji huu hasa katika kipindi hiki ambacho tamko limetolewa mpaka kipindi cha ukomo ili wajiwekee mazoea.
"Hii ni hatua kubwa Tanzania inataka kuipiga nawapongeza kwa kuanza kuendelea kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi lakini pia kuongeza ustawi kwa wananchi wake. Lakini ni wakati wa kujifunga wajibika kwelikweli" anamaliza Jacquline Masawe.
Kwa upande wa serikali ya Tanzania kauli hii si tu kwaajili ya mazingira lakini pia swala la afya.
Serikali hiyo kupitia waziri wake wa mazingira imefafanua kuwa matumizi ya kuni na mkaa yanaathiri afya ya mtumiaji kwa kusababisha magonjwa yatokanayo na kuvuta hewa chafu ambayo huathiri mapafu, moyo na matumizi ya muda mrefu ya nishati hiyo pia husababisha magonjwa ya macho,.
Ripoti ya Tatu ya Hali ya Mazingira nchini Tanzania ya mwaka 2019 inaonesha kuwa kasi ya uharibifu wa misitu ni kubwa na kila mwaka zaidi ya hekta 469,420 huharibiwa kutokana na ukataji wa miti kwa ajili ya matumizi ya kuni na mkaa.
Hata hivyo serikali ya Tanzania inasema kuwa imejipanga kujenga uchumi wa viwanda, hivyo matumizi ya nishati mbadala ikiwemo mkaa mbadala yatatoa fursa kwa viwanda vya kutengeneza mkaa mbadala sanjari na kuzalisha majiko sanifu na banifu kwa ajili ya matumizi ya nishati hiyo.