Na Coletta Wanjohi
Istanbul, Uturuki
Kila mwezi wa Septemba viongozi wa nchi tofauti duniani husafiri hadi New York nchini Marekani kwa ajili ya kuhudhuria kikao cha kila mwaka cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Na mwaka huu siku sita za hotuba za viongozi wa dunia katika kikao cha 79 zitaanza leo Septemba 24 hadi Septemba 30.
Kwa kawaida huwa ni fursa ya kila kiongozi kuongea na kupaza sauti kuhusu masuala ambayo yanatakiwa kupewa kipaumbele duniani. Kuna nchi 193 za Umoja wa Mataifa.
Mwaka huu baadhi ya viongozi wa nchi 87, makamu wa marais watatu, wana wafalme wawili, wakuu wa serikali 45, manaibu wakuu wa serikali wanane, mawaziri 45 na wakuu wanne wa nyadhifa za chini wanatarajiwa kulihutubia Baraza Kuu.
Na kwa nchi za Afrika, baadhi ya marais wametuma wawakilishi wao.
Nchi hizo ni pamoja na Sudan Kusini, Tanzania, Uganda, Rwanda, Burundi, Zimbabawe na Nigeria.
Kaulimbiu ya mwaka huu ni: "Tusimwache mtu nyuma: tushirikiane kwa ajili ya kuendeleza amani, maendeleo endelevu na utu wa binadamu kwa vizazi vya sasa na vijavyo."
Mikutano ya Baraza Kuu imefanyika tangu kuanzishwa kwake mwaka 1946 ikiwa na wajumbe 51.
Katika utamaduni ambao umedumishwa tangu 1955, Brazil siku zote imekuwa ndio ya kwanza kuhutubia Bazara hilo.
Maafisa wa UN wanadai kuwa desturi hii imedumishwa kwa sababu katika miaka ya mwanzo ya UN, Brazil ilijitokeza kuzungumza kwanza wakati nchi nyengine zilisita kufanya hivyo.
Baada ya Brazil, nchi mwenyeji, Marekani, itachukua nafasi ya pili na baadaye viongozi wengine watafuata. Kitakachozingatiwa ni pamoja na cheo cha mwakilishi wa nchi.
Hata hivyo, mikutano hii imekuwa na visa visivyo vya kawaida ambavyo vimekuwa vikikumbukwa. Kwa mujibu wa sheria, viongozi wanatakiwa kulihutubia baraza kwa dakika 15, ingawa kanuni hii mara nyingi imekuwa ikivunjwa.
Mada zinazowasilishwa, mara nyingi hugusiwa masuala mbalimbali yaliyojiri katika kipindi cha mwaka huo.
Hata hivyo, kulingana na rekodi za Umoja wa Mataifa, moja ya hotuba ndefu zaidi iliyowahi kutolewa wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu ilikuwa ya kiongozi wa Cuba Fidel Castro mwaka 1960 - alizungumza kwa muda wa saa nne na nusu.
Na mwaka 2009 kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi alizungumza kwa zaidi ya saa moja na nusu.
Wakati mwengine muhimu katika historia ya Baraza Kuu ni pale Rais wa zamani wa Umoja wa Kisovieti Nikita Khrushchev alipogonga meza kwa ngumi yake na kuigonga kwa kiatu chake baada ya kukasirika wakati wa hotuba ya Ufilipino mnamo 1960.
Hotuba ya Rais wa zamani wa Venezuela Hugo Chavez ya mwaka 2006 pia inarudiwa mara kwa mara, ambapo alimuita Rais wa zamani wa Marekani George W. Bush, "shetani."
Mnamo mwaka wa 2018, Waziri Mkuu wa wakati huo wa New Zealand, Jacinda Ardern alihudhuria Mkutano Mkuu na mtoto wake wa miezi 3.
Mwaka wa 2017 Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump katika hotuba yake alisema kwamba "angeiangamiza Korea Kaskazini," ikilazimika kufanya hivyo.
Mwaka huu, mada kuu zitajikita katika migogoro inayoendelea sehemu mbalimbali za dunia, bila kusahau changamoto za mabadiliko ya tabia nchi na nyenginezo.
Tusubiri tuone, iwapo mpaka Septemba 30, kama kutaibuka vituko vyengine ambavyo vitaingia katika historia ya jukwaa hilo la kimataifa.