"Wabunge wa Kenya wanapanga kuanzisha muswada bungeni wa kumtimua Naibu Rais wa nchi hiyo Rigathi Gachagua, wakimtuhumu kwa kuhujumu serikali," amesema kiongozi wa walio wengi bungeni, jambo linaloakisi mpasuko mkubwa kati ya viongozi hao wawili.
"Ni kweli kuna hoja ya kumtimua naibu Rais na kama mbunge wa enoa la Kikuyu, tayari nimetia sahihi," Kiongozi wa wengi bungeni Kimani Ichung'wah alisema Jumapili.
"Nitaunga mkono hoja hiyo ya kuondolewa madarakani ili kusitisha mchakato ambapo serikali inahujumiwa kutoka ndani ya serikali," alisema.
Lakini Katiba ya Kenya inasemaje kuhusu kumtimua Naibu Rais?
Naibu Rais Rigathi Gachagua na Rais William Ruto waligombea urais katika uchaguzi wa mwaka 2022 kupitia chama cha UDA na wakaibuka washindi.
Alipomteua mwaka 2022, Ruto alimtaja Gachagua kama mtu aliyejitengenezea barabara ya siasa mwenyewe, mwanasiasa mashuhuri, na mtumishi wa umma ambaye lengo lake kuu lilikuwa kusaidia wengine.
Kikatiba Rais hana uwezo wa kumfuta kazi Naibu wake.
Katiba ya Kenya inasema Naibu Rais wa nchi hiyo anaweza kuondolewa kwa lazima kwa sababu tofauti.
- Kwa msingi wa ukiukaji mkubwa wa masharti ya Katiba hii au sheria nyingine yoyote.
- Kuwepo kwa sababu kubwa za kuamini kwamba Naibu Rais amefanya uhalifu chini ya sheria ya kitaifa au kimataifa.
- Utovu wa nidhamu uliokithiri
- Ikiwa hajiwezi kimwili au kiakili kutekeleza majukumu yake.
Kumtimua Naibu wa Rais kwa sababu ya kukiuka sheria
Kifungu cha 145 cha katiba ya Kenya kinasema kuwa mjumbe wa Bunge anaweza kutoa hoja ya kumshtaki Naibu Rais ikiwa angalau theluthi moja ya wajumbe wataunga mkono.
Sababu hizo ni pamoja na ukiukaji mkubwa wa sheria, utovu wa nidhamu uliokithiri, au shutuma nzito za uhalifu.
Mara tu hoja hiyo itakapoidhinishwa, Spika wa Bunge la Kitaifa lazima amjulishe Spika wa Seneti, na kikao cha Seneti kitafanyika ndani ya siku saba.
Seneti inaweza kuunda kamati maalumu ya wanachama 11 kuchunguza madai hayo.
Naibu Rais ana haki ya kufika mbele ya kamati wakati wa uchunguzi. Kamati hiyo ina siku kumi kuwasilisha matokeo yake kwa Seneti.
Iwapo angalau thuluthi mbili ya Bunge la Seneti itapiga kura kuunga mkono mashtaka, Naibu Rais anaweza kuondolea.
Kuondolewa kwa sababu ya kukosa uwezo wa kiakili au kimwili
Hoja ya kuchunguza uwezo wa Naibu Rais kimwili au kiakili inaweza kutolewa na mjumbe wa Bunge kwa kuungwa mkono na angalau robo ya wajumbe wote.
Iwapo walio wengi bungeni wataunga mkono hoja hiyo, Spika lazima amjulishe Jaji Mkuu ndani ya siku mbili.
Jaji Mkuu anahitajika, ndani ya siku saba, kuteua joto la watu watano kuchunguza kesi hiyo.
Mahakama hii itajumuisha madaktari watatu waliopendekezwa na chombo cha kitaaluma, wakili mmoja wa Mahakama Kuu, na mtu mmoja wa ziada aliyependekezwa na Rais (au mwanafamilia wa karibu ikiwa Rais hawezi kuteua).
Ndani ya siku 14, mahakama lazima itoe ripoti ya matokeo yake kwa Jaji Mkuu na Spika, ambaye atawasilisha ripoti hiyo kwenye Bunge ili kupigiwa kura.
Iwapo mahakama hiyo itathibitisha kuwa Naibu Rais hawezi kutekeleza majukumu yake, na wabunge wengi wakapiga kura ya ndiyo, Naibu Rais atavuliwa madaraka yake.