‘’Moyo wangu ni mwepesi… Umenikalia chapat… Nafanya vituko kama chizi ... Kukupenda sitasizi... Sura yako muzuri mama…’’
Yaani ukitamka maneno hayo katika mtaa wowote Afrika Mashariki, utasikia mtu akiungana nawe kuimba na hata kucheza densi
Ni kwasababu huu ni wimbo maarufu sana wa bendi ya Sauti Sol uliopewa jina ‘Sura Yako.’ Ambao katika mtandao wa YouTube umepata kutazamwa zaidi ya mara milioni 15.
Wimbo huo unasikika kwa umbali katika studio ya William Tuva, anako peperushia kipindi maarufu Afrika Mashariki cha ‘Mambo Mseto’ kinachoangazia muziki wa Afrika.
‘‘Sauti Sol ni vijana wa maajabu tu. Namna sauti zao zinaendana, muziki wao unakubeba.’’ Tuva ameambia TRT Afrika. ‘‘Nimewaona hawa vijana tangu wakianza muziki wao hadi kuwa mojawapo ya bendi kubwa zaidi Afrika.’’ Ameongeza.
Kundi hilo kutoka Kenya, Sauti Sol, lilianzishwa na maswahiba 2005, na bingwa wa sauti Bien-Aimé Baraza, Willis Chimano anayevutia zaidi kwa weledi wake wa kuimba sauti ya chini, Mchunaji gita Polycap Otieno na gwiji wa utunzi Savara Mudigi ambapo wamevutia mamilioni wa mashabiki kote Afrika.
Lakini ni kama vile muda umewadia kwa kundi hilo kupungia mkono jukwaa, huku wakiahidi mashabiki wao kuwa wataanza kurusha vitu kama wasanii binafsi.
Bendi zina nafasi yao Afrika
Mabendi yanapovunjika mara nyingi inazungumziwa kwa minong’ono. Hii ni kutokana na kuwa wengi wao wanatengana kwa ubaya na chuki, au wakati mwingine katika mazingira tete au hata wanaweza kutengana na usijue kabisa sababu.
La hakika ni kuwa, kila linapovunjika kundi moja, hakukosi kundi lingine linaloibuka na kuvuma.
Mtaalamu wa mahusiano na mauzo ya wasanii kutoka Kenya, Anyiko Owoko, anaamini siku zote kutakuwa na hamu ya mabendi Afrika, kwani bara linatamani muziki huo.
‘‘Mbali na makundi machache hapa na pale, hakuna mabendi ya kutosha.’’ Anaongeza. ‘’ Sekta hiyo ipo tayari na itafaidika kikweli na kutokea mabendi kama haya. Sijawahi kuona bendi lililoibuka na likakosa wafuasi.’’
Katika miaka ya nyuma, makundi mengi yamewahi kutokea barani Afrika kisha yakadidimia ghafla, yakiwaacha mashabiki na hamu zaidi. ‘’Inaridhisha zaidi kufuata muziki wa bendi kuliko wa msanii binafsi. Wanakuwa na mashamsham mengi zaidi. Ni mseto wa talanta zinazovutia.’’
Kwanini mabendi hayaonekani kudumu?
Saidi Fella, anasifika kwa kuanzisha na kusimamia bendi maarufu ya vijana Tanzania, Yamoto Band. Bendi hiyo imetawanyika japo wasanii husika wameibuka kuwa wasanii wakubwa binafsi Afrika Mashariki.
Saidi anasema ni vigumu sana kuliweka kundi lililo na wabunifu huru pamoja kwa muda mrefu.
‘‘tunakuta kuna memba mmoja anayetaka kuwapiku wenzake kwa umaarufu.’’ Anaeleza. ‘’ Baadhi hawataki kuzingatia maoni ya wengine. Wanataka kufanya maamuzi yote peke yao. Hili haliwezekani katika makundi.’’
Lakini meneja wa talanta Owoko anahisi kuwa wakati mwingine tofauti hizi ndizo zinayapa makundi haya nguvu.
‘‘Unaweza kuta mmoja ni shupavu wa utunzi, mwingine ni hodari katika mavazi na mitindo na mwingine pengine mweledi katika kucheza zana. Unachohitaji kufanya ni kuonesha uzuri wa kila mmoja ili wote wahisi kuwa wana nafasi sawa.’’
Ni kama kuwa katika ndoa
Ali Suleiman, ni mwanzilishi wa kikundi cha Lafrik. Anasema kuwa ndani ya bendi ni rahisi, ila unahitaji kuweka juhudi.
‘‘Ni kama vile kuwa katika ndoa. Baadhi hufaulu na zingine zinavunjika. Lazima mjifundishe kuvumiliana. Muwe na maelewano. Lazima mfanyie kazi hilo,’’ anasema.
Lafrik wamekuwa pamoja kwa miaka 9. Suleiman anasema ameshuhudia namna muziki wa bendi umeendelea kupata umaarufu miongoni mwa vijana.
‘‘Wanatupokea vyema sasa. Nimewahi kufanya kazi na mabendi ya wazee kama vile Les Wanyika. Maarufu sana. Nimeona vijana wengi wakijitokeza katika tamasha zetu na wanajaza ukumbi kabisa.’’
Ufanisi wa kuvuka mipaka
Makundi mengi yanaweza kupima ufanisi wake kutokana na namna wanapokewa nje ya nchi zao.
‘‘Sisi ndio tumerudi tu kutoka Tanzania mwezi Aprili. Nilifurahi sana kauona walivyotupokea,’’anasema Suleiman.
Licha ya changamoto wanazokabiliana nazo makundi haya, fani ya muziki inaendelea kukua kwa kasi barani Afrika.
Utofauti wa tamaduni, sauti, mavazi na hali ya maisha, zinawapa wasanii mada nyingi za utunzi. Wataalamu wanasema kuwa sekta ya muziki inatarajiwa kukua kwa mamia ya milioni ya madola kufikia 2025.
Kwa mujibu wa mtaalamu wa burudani na mauzo ya wasanii Owoko, makundi mengi yanapwaya pale wanapokosa wasimamizi waadilifu.
‘‘Makundi yanatakiwa kuwa na wasimamizi wachache iwezekanavyo. Kuwa na mameneja wengi sio jambo la busara. Kila mmoja atakuwa analipwa na unakuta wakati mwingine pesa zinazotumiwa kuwalipa meneja ni nyingi kuliko pesa za kuwalipa wasanii.’’
Mitandao ya kijamii imeonesha kuwa muziki wa kiafrika, hasa unaposukwa vyema, unaweza kuwavutia mashabiki wengi hata nje ya bara. Wimbo kama vile ‘Jerusalema’ kutoka Afrika Kusini ulipokewa vikubwa ajabu.
Amapiano ndio mtindo unaovuma zaidi kwa sasa kote duniani na imepata mashabiki wa kila tabaka. Mtaalamu Owoko anasema kuwa hii ni ishara kuwa mashabiki wa muziki kule nje wanasubiri kuona kwa hamu nini kitatokea Afrika tena.
‘’Amapiano ilipotokea, hakuna aliyetarajia itaunganisha ulimwengu hivyo. Na ilisambaa nje ya Afrika ,’’ anasema. ‘’ Sijui nini kipya kinakuja, ila nina uhakika kitu kizito kinapikika.’’
Gwiji wa gita na uimbaji Suleiman anatabasamu akifikiria mambo wanayopanga. Bendi yake Lafrik inajiandaa kwa tamasha nje ya Kenya, wanakoishi sasa.
‘‘Watu wanataka kuonja muziki wetu kutoka nchi jirani. Inaonesha kuwa kuna fursa nzuri ya kukuahata mbali na nchi yako,’’ anasema. ‘’Baadhi ya makundi haya yanaishia kukaa nje zaidi ya kuwa ndani ya nchi zao.’’
Mtangazaji maarufu Tuva anasema kuwa huenda Sauti Sol wanapumzisha kikundi, ila makundi mengine mengi yapo na yatatokea tu na kuwashangaza wengi.
‘‘Nimefanya kazi na makundi mengi sana. Siwezi kusahau makundi Yamoto Band kutoka Tanzania. Walitupatia majina makubwa sana yaliyobadili taswira ya mzuki wa bongo fleva.’’ Anaongeza. ‘’Nawavulia kofia bendi ya H_art the Band. Sijui wamewezaje kukaa pamoja muda wote huu. Lakini nina uhakika kuna wengine wengi wanakuja.’’