Na Emmanuel Onyango
Kwa Wahaiti, pendekezo la Kenya kuongoza kikosi cha kimataifa kurejesha utulivu nchini linasikika kuwa la kawaida sana.
Ardhi yao inakabiliwa na ghasia za magenge na ukosefu wa utulivu wa kisiasa. Baada ya miezi kadhaa ya ghasia zinazoongezeka, familia zimekimbia kutoka kwa magenge yanayodhibiti sehemu kubwa za nchi.
Wakati huo huo, makundi ya walinda usalama katika mji mkuu uliokumbwa na ghasia Port-au-Prince wamechukua mapanga na marungu ili kupigana
Hata hivyo, hawajaweza kufanikiwa kukabiliana na magenge ambayo yamejihami kwa silaha za mashambulio hasa kutoka Marekani, kulingana na ripoti. Makundi yenye silaha pia yamewapiga risasi polisi wa eneo hilo.
Magenge yamekuwa yakisababisha ukosefu wa usalama nchini Haiti kwa miongo kadhaa. Bado, ghasia zimezidi kuwa mbaya tangu kuuawa kwa Rais Jovenel Moise mnamo 2021, na kusababisha pengo la madaraka na kuacha vikundi vyenye silaha viking'ang'ania udhibiti.
Vurugu hizo zikiwemo za utekaji nyara kwa lengo la kulipwa fidia, zimeharibu miundombinu na kuharibu huduma muhimu kama vile afya na elimu.
Mwaka huu pekee, Wahaiti 2,400 wameuawa na mamia ya wengine kutekwa nyara, kulingana na Umoja wa Mataifa.
Kenya imesikia malalamiko
Kwa jinsi mambo yalivyo, Haiti bado haijachagua wawakilishi baada ya muda wa maseneta kukamilika mwezi Januari.
Huku kukiwa na uvunjaji sheria, Waziri Mkuu wa Haiti Ariel Henry aliomba uingiliaji kati wa kimataifa ili kurejesha utulivu nchini humo. Alipata kuungwa mkono na Umoja wa Mataifa, Marekani, na washirika wake.
Kufuatia kutiwa saini kwa mkataba na Marekani mapema wiki hii, Kenya imekubali kutuma kikosi cha polisi 1,000 kuingilia kati ili kusaidia kuondosha magenge hayo na kuleta amani.
Marekani inatarajiwa kufadhili upelekaji. Pendekezo hilo linasubiri kuidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Rais wa Kenya William Ruto alisema serikali yake inaitikia wito wa Haiti wa usaidizi na kwamba ujumbe huo ni mradi wa Waafrika wote katika mshikamano na Wahaiti.
Majukumu yaliyoainishwa ya kikosi hicho ni kulinda mitambo, kutoa usaidizi wa uendeshaji dhidi ya magenge na kutoa mafunzo kwa polisi wa Haiti.
“Kilio cha ndugu na dada zetu kimefika masikioni mwetu na kugusa mioyo yetu,” Ruto aliambia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Kenya na matatizo yake ya ndani
Waziri wa Mambo ya Nje Alfred Mutua aliwaambia wanahabari wiki jana kuwa huenda mataifa mengine ya Afrika yakaijiunga katika oparesheni hiyo.
Hata hivyo, wachambuzi wana hisia tofauti kuhusu misheni hiyo. Wengine wanahoji kuwa inalenga azma ya Kenya ya kuinua hadhi yake katika jukwaa la kimataifa lakini kwa gharama ya kuonyesha maslahi ya Marekani kufuatia ripoti za ugumu wa awali wa kuajiri kikosi cha kimataifa kinachoungwa mkono na Marekani kwa Haiti.
"Mawazo ni makosa, mawazo ni makosa. Kwanza, ukosefu wa uwezo ni suala. Pili ni utegemezi wa nia njema ya baadhi ya vikosi vya kigeni," Prof Munene Macharia, mtaalamu wa uhusiano wa kimataifa anayeishi katika mji mkuu, Nairobi, aliambia. TRT Afrika.
Kenya ina mahitaji yake ya usalama ambayo hayajatimizwa huku ikikabiliwa na mashambulizi ya mara kwa mara ya kundi la kigaidi la Al-Shabab lenye makao yake katika nchi jirani ya Somalia.
Mashambulizi ya kundi hilo yamechacha katika miezi ya hivi karibuni, huku zaidi ya matukio 90 ya ghasia yakirekodiwa katika eneo la mpaka yakilenga vikosi vya usalama na raia, kulingana na ripoti ya Mradi wa Data ya Mahali pa Migogoro na Matukio (Acled).
Kuchunga heshima ya Wahaiti
Waangalizi wa haki za binadamu kwa muda mrefu wamekuwa wakishutumu jeshi la polisi la Kenya kwa kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya raia wakati wakijaribu kutatua changamoto za kiusalama. Polisi mara nyingi hukanusha shutuma hizo na kusisitiza uwajibikaji wa hali ya juu.
Huko Haiti, kuna upinzani mkubwa wa ndani wa kupeleka jeshi lolote la kimataifa. Viongozi wa magenge wameonya kwamba watapambana na jeshi lolote la kimataifa litakalotumwa nchini humo. Itakuwa vita kuokoa "heshima na nchi" yao, mmoja wao aliwaambia waandishi wa habari wa kimataifa mwezi uliopita.
Wakati wa ujumbe wa awali wa Umoja wa Mataifa nchini Haiti kati ya 2004 na 2017, askari wa kigeni walituhumiwa kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu, na baadhi ya Wahaiti bado wana kumbukumbu za uhalifu huo unaodaiwa.
"Kwa watu wa Haiti, itakuwa hisia mseto. Juhudi za kulinda amani katika siku za nyuma zimekuwa na ukiukwaji mwingi wa haki za binadamu na changamoto zote zinazoletwa na kutuma jeshi la kulinda amani katika nchi kama hiyo," alisema Adam Bonaa, mchambuzi wa masuala ya usalama wa Afrika anayeishi nchini Ghana.
Changamoto ya lugha
Hata hivyo, anaamini bado kuna matumaini. "Lazima tuipe serikali ya Kenya na nchi za Magharibi nafasi yao, tukitumai kwamba wakati huu, mambo yatafanyika sawa. Hatuwezi kutupa mikono yetu kwa kukata tamaa na kusema kwamba masuala ya Haiti hayawezi kurekebishwa," aliiambia TRT Afrika.
Lakini pia kuna suala la kizuizi cha lugha. Kenya ni taifa linalozungumza Kiingereza, na maafisa wake wa polisi wanatumwa miongoni mwa watu wanaozungumza Kifaransa karibu milioni 11. Wataalamu wanasema hii inaweza kufanya shughuli zao kuwa ngumu zaidi.
"Hawazungumzi lugha ya Krioli ya Haiti, na hawajui eneo," alisema Prof Jemima Pierre, msomi wa Haiti ambaye anafundisha masomo ya Afrika na Afro-Amerika huko California.
"Je, unafikiri kuleta jeshi la watu ambao hawazungumzi lugha hiyo, ambao hawajui hali halisi nchini Haiti, unafikiri itaifanya kuwa bora zaidi?"
Baadhi ya wafafanuzi wanapendekeza kwamba mwanzo bora utakuwa kwa Kenya kutekeleza kikosi kidogo kulingana na kile ambacho baadhi ya mataifa ya Caribean yanayojiunga na uingiliaji kati yanapeleka.
Wachambuzi wengine wanasema kilicho muhimu zaidi kwa Haiti ni uungwaji mkono katika kujenga upya kikosi chake cha polisi kisichokuwa na wafanyakazi na vifaa duni na kuanzisha upya miundo ya kisiasa ili kukabiliana na magenge hayo badala ya awamu nyingine ya kutumwa kwa vikosi vya usalama vya kigeni.