Mchezaji nyota wa zamani wa Timu ya Taifa ya Voliboli, Kenya Janet Wanja amefariki / Picha : Rais William Ruto X

Mchezaji nyota wa zamani wa Timu ya Taifa ya Voliboli, Kenya Janet Wanja amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 40.

Kifo cha Wanja kilithibitishwa na jamaa zake siku ya Alhamisi, Disemba 26 jioni.

Mchezaji huyo wa zamani ambaye alikuwa anahudumu kama kocha wa Timu ya Taifa ya Malkia Strikers aliugua saratani ya kibofu cha mkojo.

‘’Familia ya Janet Wanja ingependa kuwatangazia kuwa amefariki dunia baada ya kuugua saratani’’ taarifa kutoka kwa kaka yake Kevin Kimani ilisema.

Wanja alijiunga na benchi la ufundi la Timu ya Taifa ya Voliboli mapema mwaka huu baada ya kustaafu kama mchezaji.

Alikuwa na kikosi hiko katika mashindano ya Olimpiki ya Paris, nchini Ufaransa. Akiwa mchezaji alicheza katika vilabu vya KCB na Kenya Pipeline.

Katika salamu zake za rambirambi Rais William Ruto amemtaja Janet Wanja kama mchezaji nyota na mzalendo.

‘’Alikuwa mchezaji mahiri na mwenye nidhamu ambaye alitumikia taifa lake kwa uzalendo na heshima kubwa, siku moja tutaishinda saratani. Lala salama Wanja, ’’ alisema Rais Ruto kwenye mtandao wa X.

Rais wa Shirikisho la Voliboli nchini Kenya Charles Nyaberi pia aliomboloza kifo cha Janet Wanja.

"Shirikisho la Voliboli linaskitika kutangaza kifo cha nyota wetu mpendwa, Janet Wanja Mungai. Mchango wa Janet kwa Shirikisho na michezo kwa jumla ulikuwa wa aina yake,’’ alisema Nyaberi.

Wanja ameshinda mataji kadhaa barani Afrika akiwa na timu ya taifa kama mchezaji, na pia akiwa na klabu ya Kenya Pipeline.

TRT Afrika