Jamhuri ya Congo yazuia safari za mawaziri hadi mwisho wa mwaka 2024

Jamhuri ya Congo yazuia safari za mawaziri hadi mwisho wa mwaka 2024

Nchi hiyo imeweka katazo hilo litakalodumu mpaka mwisho wa mwaka 2024.
Rais wa Jamhuri wa Congo Denis Sassou Nguesso./Picha: AFP

Jamhuri ya Congo imesitisha safari za mawaziri na maofisa nchini humo hadi mwishoni mwa mwaka, serikali ya nchi hiyo imesema siku ya Jumatano.

"Safari zote za nje za mawaziri na maofisa wengine wa serikali zenye kutumia fedha za umma zimesitishwa mpaka mwisho wa mwaka 2024," ilisema taarifa ya Waziri Mkuu wa nchi hiyo Anatole Collinet Makosso.

"Ruhusa maalumu itatolewa tu kwa safari zinazomhusu Rais wa Jamhuri," ilisema nakala ya taarifa hiyo kama ilivyonukuliwa na AFP.

Changamoto za kifedha

"Hatua hiyo inalenga kupunguza gharama za serikali, ambayo inakabiliwa na changamoto kubwa ya kifedha ", chanzo cha serikali kiliiambia AFP.

"Sehemu kubwa ya uchumi wa Congo imekuwa ikipitia changamoto kubwa ya kifedha," kilisema chanzo hicho.

Jamhuri ya Congo, ambayo inasifika kwa kuzalisha mafuta kwa wingi, inakadiriwa kuwa na watu milioni sita.

Hata hivyo, kulingana na benki ya dunia, nusu ya idadi ya watu hao wanaishi kwenye dimbwi la umasikini.

TRT Afrika