Bodi kuu ya Shirika la Fedha la Kimataifa, IMF, imetia saini karibu dola bilioni 1 za ufadhili mpya kwa Kenya.
IMF ilisema bodi hiyo ilikamilisha ukaguzi wa tano chini ya 'Mfuko wa Upanuzi wa Hazina' ya Kenya na usaidizi wa kuongeza mikopo, na kuruhusu takriban dola milioni 415.4, kutolewa mara moja.
Pia iliamua kuongeza mipango hiyo hadi miezi 48 kutoka 38 ili kuipa Kenya muda zaidi wa kutekeleza mageuzi.
Pia iliidhinisha mpango mpya wa miezi 20 wenye thamani ya takriban dola milioni 551.4 ambao utasaidia juhudi za Kenya kustahimili athari ya mabadiliko ya tabianchi.
Mageuzi ya Uchumi
IMF ilisema Kenya imepata maendeleo mazuri katika kutekeleza mageuzi ya kiuchumi licha ya kukabiliwa na ukame mbaya zaidi kuwahi kutokea kwa miongo kadhaa, pamoja na mazingira magumu ya nje.
Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa IMF Antoinette Sayeh alisema hatua za Jumatatu zitaruhusu mamlaka ya Kenya kuendelea kushughulikia changamoto kama hizo, kudumisha imani ya soko, kukuza ukuaji na kuendeleza mageuzi yanayoendelea.
Alisema kuidhinishwa kwa bajeti ya Kenya ya mwaka wa 2023-2024 na Sheria ya Fedha ya 2023 ni "hatua muhimu" zinazohitajika kusaidia juhudi zinazoendelea za ujumuishaji na kupunguza udhaifu wa deni wakati wa kulinda matumizi ya kijamii na maendeleo.
Masharti magumu ya ufadhili pia yalihitaji "sera ya busara ya madeni" na kuendelea na juhudi za kuweka kipaumbele cha mikopo yenye masharti nafuu, alisema.
Mkopo wa Burundi
Bodi ya IMF pia imeidhinisha Msaada wa Mikopo Ulioongezwa wa $271 milioni kwa Burundi, na kulipwa mara moja zaidi ya $62 milioni.
Uchumi wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki ndio kwanza unaanza kuimarika kutokana na mzozo wa miaka mingi na msukosuko wa kisiasa chini ya kiongozi wa zamani Pierre Nkurunziza ambao uliacha sekta kuu zikiyumba.
IMF ilisema mkopo huo utasaidia kushughulikia deni ya muda mrefu na mahitaji ya malipo ya Burundi, kujenga upya akiba za nje na kuunga mkono ajenda ya mageuzi ya serikali.