Na Edward Qorro
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki
Bara la Afrika lina jumla ya faru 23,885, utafiti uliofanywa na taasisi ya International Rhino Population (IRF), unaonesha.
Kulingana na utafiti huo, uliotolewa hivi karibuni, bara la Afrika lina jumla ya faru weupe 17,464 huku idadi ya faru weusi ikiwa ni 6,421.
Utafiti wa IRF unaonesha kuwa ujangili wa faru barani Afrika uliongezeka kwa asilimia nne kwa mwaka kutoka mwaka 2022 hadi 2023.
Wakati huo huo, kila baada ya saa 15, majangili waliua faru 586 katika kipindi cha mwaka 2023, kwa mujibu wa IRF.
"Wakati maeneo mengine yakishuhudia ongezeko la faru weusi, hali imekuwa tofauti mwaka jana, kutokana na ujangili uliokithiri nchini Namibia na ndani ya hifadhi ya taifa Hluhluwe iMfolozi iliyoko Afrika Kusini," sehemu ya ripoti hiyo inasema.
Hata hivyo, Afrika Kusini inaendelea kushuhudia ongezeko la idadi ya faru weupe, licha ya kukithiri kwa vitendo vya ujangili.
"Ninaona faraja sana kushuhudia ongezeko la faru Afrika," anasema Dkt Dave Balfour, ambaye pia ni mtaalamu wa faru kutoka IUCN. "Hiki ni kiashirio tosha kuwa licha ya tishio la ujangili, nchi nyingi ziko tayari kulinda na kuhifadhi viumbe hawa wa ajabu. Maadamu vifaru wanathaminiwa na watu, tuna nafasi ya kuzuia kufa kwao."
Pamoja na mambo mengine, ujangili dhidi ya faru huchochewa na mahitaji ya ‘pembe’ yake, katika nchi nyingi za bara la Asia, hususani China ambako hutumika kama dawa ya kienyeji, lakini pia kama ishara ya hadhi na utajiri.
Licha ya kuongoza kwa idadi kubwa ya faru, Afrika Kusini ndio kinara wa matukio ya ujangili dhidi ya mnyama huyo.
Kulingana na utafuti wa IRF, jumla ya faru 499 waliuwawa na majangili nchini Afrika Kusini, katika kipindi cha mwaka 2023.
Namibia inashika nafasi ya pili kwa kuwa na faru 3,612. Nchi hiyo ilishuhudia faru 67 wakiuwawa na majangili ndani ya mwaka 2023.
Kenya ni ya tatu, na ndio kinara wa idadi ya faru kwa ukanda wa Afrika Mashariki. Nchi hiyo ina jumla ya faru 1,811, ambapo 938 ni weusi wakati weupe ni 873.
Hata hivyo, Kenya ilishuhudia faru mmoja akiuwawa mwaka 2023.
Zimbabwe inashika nafasi ya nne ikiwa na faru 1,033, ambapo jumla ya faru 11 waliuwawa katika kipindi cha 2023.
Tanzania ni ya sita kwa Afrika, baada ya Botswana. Nchi hiyo, ambayo ilijizoelea umaarufu kupitia faru Fausta, ina jumla ya faru 212 kulingana na utafiti huo, ambapo pia haijashuhudia ujangili dhidi ya faru kwa kipindi cha miaka miwili.
Fausta, ambaye anaaminika kuwa ndiye faru jike mzee zaidi duniani, alifariki mwaka 2019, akiwa na umri wa miaka 57.
Fausta aliishi maisha yake yote katika Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), na iliwalazimu wahifadhi wa NCAA kumuweka kwenye kibanda maalumu, baada ya mnyama huyo kupata upofu.
Faru ni miongoni mwa wanyama wakubwa watano wakiwamo tembo, Simba, Nyati na Chui.
Mwezi Juni mwaka huu, Wizara ya Maliasili na Utalii ya Tanzania ilisema kuwa idadi ya faru iliongezeka kutoka 161 mwaka 2019 hadi kufikia 253 mwaka 2023 kutokana na teknolojia ya ulinzi, ijulikanayo kama ‘Transmitters’.