Msako wa Kenya wa kuwatafuta manusura wanaohusishwa na ibada katika eneo la pwani ya nchi hiyo utaenea hadi katika Hifadhi ya Kitaifa ya Tsavo Mashariki, Waziri wa Mambo ya Ndani Kithure Kindiki alisema.
Inafuatia ugunduzi wa mwezi uliopita wa makaburi ya halaiki katika msitu wa Shakahola kaunti ya Kilifi ambapo mamlaka imefukua miili 235 hadi sasa, huku mamia ya watu wanaohusishwa na kanisa la Good News International wakiwa bado hawajulikani walipo, kwa mujibu wa shirika la msalaba mwekundu la Kenya.
Takriban watu 90 wanaoaminika kuwa waumini wa kanisa hilo wameokolewa tangu makaburi hayo kugunduliwa - wengine wakiwa katika hali mbaya. Mamlaka inashuku watu wengi zaidi wanaweza kujificha katika mbuga hiyo ya kitaifa - mbuga kubwa zaidi nchini ambayo ni maarufu kwa simba wake, ndovu na nyati.
Msako na uokoaji wa manusura katika mbuga hiyo utahusisha matumizi ya doria za ardhini na upekuzi wa ndege zisizo na rubani, Bw Kindiki alisema kwenye taarifa.
Familia za jamaa waliopotea zimekuwa zikitoa wito kwa ndege hiyo kutumika katika operesheni ya utafutaji, gazeti la ndani la Daily Nation linaripoti.
Utoaji wa miili hiyo pia umesitishwa ili kuruhusu mipango ya uchunguzi wa miili 123 iliyopatikana wiki jana. Uchunguzi wa upasuaji wa maiti utaanza Jumatano na kutafuta makaburi mengine kutaanza tena hivi karibuni, alisema waziri huyo.
Kiongozi wa kanisa hilo, Paul Mackenzie Nthege, yuko chini ya ulinzi wa polisi pamoja na mkewe na washukiwa wengine zaidi ya 30. Mamlaka imesema atashtakiwa kwa makosa yanayohusiana na ugaidi.