Juma Issihaka
TRT Afrika, Dar es Salaam, Tanzania
Chama Cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania, kimempitisha Dk Emmanuel Nchimbi kuwa Katibu Mkuu wake, akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Daniel Chongolo aliyejiuzulu wiki sita zilizopita.
Kujiuzulu kwa Chongolo, kulitokana na kile alichoandika katika barua yake Novemba 27 mwaka jana kuwa, amelazimika kuwajibika kutokana na kudhalilishwa katika mitandao ya kijamii.
Mwanasiasa huyo ameteuliwa katika Kikao cha Kamati Kuu kilichofanyika visiwani Zanzibar na jina lake kuthibitishwa na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho tawala nchini Tanzania.
Hata hivyo, uteuzi wa Dk Nchimbi katika nafasi hiyo ulitabiriwa na wadau mbalimbali wa siasa nchini Tanzania akihusishwa yeye, Martin Shigella (Mkuu wa Mkoa wa Geita), William Lukuvi (Mshauri wa Rais Siasa na Uhusiano wa Jamii) na Amos Makalla (Mkuu wa Mkoa wa Mwanza), wote ni makada wa kitambo ndani ya chama hicho.
Makada na wanadiplomasia wenzake, wanasema ni mtu sahihi kwenye nafasi hiyo kutokana na uzoefu wake wa uongozi wa CCM, kadhalika si mnafiki na hana makundi.
Historia ya Dk Nchimbi ndani ya CCM unaweza kuifananisha na umri wa mtu mzima. Ameanza kuwa kiongozi katika chama hicho mwaka 1998 alipochaguliwa kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC).
Hakuishia hapo, baadaye alichaguliwa na Wajumbe wa Baraza la Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), kuwa Mwenyekiti wao na hivyo aliiongoza jumuiya hiyo pia.
Mwaka 2005, mwanasiasa huyo alijitosha katika kinyang’anyiro cha kuwania ubunge wa Songea Mjini, alikopata ushindi wa asilimia 67.6 dhidi ya mpinzani wake mkuu kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edson Mbogoro.
Ubunge wake, ulifungua milango mingine ya nyadhifa ndani ya Serikali, Januari mwaka 2006, Rais wa wakati huo, Jakaya Kikwete alimteuwa kuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo.
Alidumu kwenye wadhifa huo kwa miezi tisa na Oktoba mwaka huo alihamishiwa Wizara ya Kazi, Ajira na Vijana akiwa na nafasi ile ile hadi Februari mwaka 2008.
Mwanasiasa huyo alihamishiwa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa akiwa Naibu Waziri, alikohudumu hadi mwaka 2010.
Kipyenga cha uchaguzi kilipopigwa mwaka 2010, aliwania tena ubunge katika eneo lile lile na alishinda na kuanzia hapo nyadhifa zake ndani ya Serikali ziliongezeka.
Rais Kikwete alimteuwa kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo hadi Mei mwaka 2012, alipohamishiwa Wizara ya Mambo ya Ndani kabla ya kuamua kujiuzulu Disemba mwaka 2013.
Msingi wa kujiuzulu kwake ni shinikizo, baada ya ripoti ya Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, iliyoongozwa na Mbunge wa Kahama, James Lembeli juu ya “Oparesheni Tokomeza.”
Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Dk Nchimbi alikuwa miongoni mwa makada wa CCM waliotangaza nia ya kuwania Urais kwa tiketi ya chama hicho. Hata hivyo John Magufuli ndiye aliyepitishwa kupeperusha bendera ya chama hicho.
Baada ya Uchaguzi huo, mwaka 2016, Dk Nchimbi aliteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Brazil kisha mwaka 2022 aliteuliwa kuiwakilisha Tanzania nchini Misri alikohudumu hadi mwaka 2023 na kurudi nchini.
Panda shuka ndani ya CCM
Machi mwaka 2017, akiwa Balozi wa Tanzania nchini Brazil Dk Nchimbi aliwahi kukumbwa na msukosuko ndani ya chama chake, akipewa onyo kali na adhabu ya kutogombea nafasi yoyote kwa kipindi cha miaka minne.
Adhabu hiyo ilitokana na kile kilichoelezwa na CCM kuwa, ni usaliti katika uchaguzi wa mwaka 2015. Hata hivyo makada wengine wa chama hicho walifutwa uanachama akiwemo aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa chama hicho (UWT), Sophia Simba.
Katika uchaguzi huo, Dk Nchimbi alijitokeza hadharani kupinga uamuzi wa CCM kumpendekeza Magufuli kuwa mgombea wake wa urais.
Wasifu zaidi
Kada huyo alizaliwa Desemba 24, mwaka 1971 mkoani Mbeya na alianza masomo katika Shule ya Msingi Oysterbay, Dar es Salaam mwaka 1980 hadi 1986.
Mwaka 1987 hadi 1989 alisoma elimu ya Sekondari katika shule ya Uru na baadaye kuhamia Shule ya Sekondari Sangu alikomalizia kidato cha nne mwaka 1990.
Kidato cha tano na sita alisoma katika Shule ya Sekondari ya Forest Hill mkoani Morogoro mwaka 1991 hadi 1993. Alijiunga katika Chuo cha IDM Mzumbe na kuhitimu Stashahada ya Juu ya Utawala 1997.
Baadaye alisoma shahada ya uzamili ya usimamizi wa biashara katika chuo hicho, mwaka 2001 hadi 2003 akibobea kwenye maeneo ya benki na fedha na mwaka 2011 alihitimu shahada ya uzamivu (PhD) katika chuo hicho.
Dk Nchimbi ni mume na baba wa watoto watatu.
Si mnafiki
Akizungumzia uteuzi huo, kada wa chama hicho, Sophia Simba amesema Dk Nchimbi ni mtu sahihi kwenye wadhifa huo kwa kuwa hana unafiki na ni muwazi.
Ameeleza CCM ilihitaji mtu kama Dk Nchimbi kwenye nafasi hiyo, akisisitiza amestahili kwa uzoefu na uwezo wake.
“Mashaallah… Sasa CCM tumepata Katibu Mkuu, anafaa kwa kuwa hana unafiki wala makundi na ni muwazi. Chama kilihitaji mtu kama yeye sio hao wanaopitapita,” amesema Sophia aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa UWT Taifa.
Ni mzoefu
Mwanadiplomasia mbobezi, Balozi Christopher Liundi amesema Dk Nchimbi ni miongoni mwa wanasiasa wenye mizizi ndani ya chama hicho kwa kuwa walianza kukitumikia kitambo.
“Nakumbuka baba yake (Mzee John Nchimbi) alikuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kigoma, wakati huo mimi nikiwa Mkuu wa Mkoa huo, kwa hiyo Nchimbi alianza mbali sana na CCM,” amesema.
Kwa uzoefu wa Dk Nchimbi, Balozi Liundi aliyewahi kuiwakilisha Tanzania nchini Ethiopia, amesema utamwezesha kukiongoza chama hicho katika dira inayostahili na kupata manufaa makubwa kwa wanachama na taifa kwa ujumla.
Lakini, amesema fani yake ya diplomasia itampa nafasi ya pekee kutumia mbinu mbalimbali za kidiplomasia kutatua matatizo mbalimbali sio tu ya wanachama bali kitaifa.
“Nina matumaini makubwa wala sina mashaka lakini la msingi ni tumsaidie, pale ambapo kutahitajika ushauri ashauriwe ili apate mafanikio mazuri kwenye kazi yake kubwa na manufaa makubwa kwa chama hicho na taifa kwa ujumla,” amesema Balozi Liundi aliyewahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa.
Wapinzani wamkaribisha
Alipotafutwa kuzungumzia uteuzi huo, Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itifaki na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema ameanza kwa kumkaribisha Dk Nchimbi katika mapambano ya kisiasa.
“Anapaswa kutambua kuwa amerithi nafasi katika chama ambacho kinaogopa mijadala ya wazi na maandamano, kwa hiyo ataamua awe hivyo au abadilike,” amesema.
Hata hivyo, Mrema amemtaka mtendaji mkuu huyo mpya wa CCM, ajiandae kukabiliana na ushindani wa hoja na sio kutumia nguvu ya dola.
“Akiamua kutumia nguvu ya dola na mabavu hatadumu kwa muda mrefu kwenye nafasi yake, kwa sababu duniani kote siasa za mabavu hazijawahi kushinda,” amesema Mrema.
Chongolo ampongeza
Katika ukurasa wake wa Instagram, aliyekuwa na wadhifa huo, Chongolo amempongeza Dk Nchimbi kwa kuaminiwa na kupewa nafasi hiyo, akisema hana mashaka naye.
“Hongera saaana Balozi Dr. Emmanuel Nchimbi kwa kuaminiwa na Mwenyekiti wa CCM Rais Samia Suluhu Hassan na kupendekeza jina lako na NEC kuridhia wewe kupeperusha bendera ya CCM kwa dhamana ya Mtendaji Mkuu, Katibu Mkuu.
“Imani ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kwako ni kubwa sana nasi wana CCM hatuna mashaka nawe. Hongera saaana na kila lakheri!,” ameandika.