Na Gaure Mdee
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki.
Serikali ya Tanzania imesisitiza kuwa haitosajili makundi ya mitandaoni katika mchakato wa kusajili vyama na makundi unaoendelea jijini Dar es Salaam.
Badala yake, Tanzania imesema kuwa zoezi hilo linalenga kuhalalisha uwepo wa baadhi ya vyama na vikundi mbalimbali katika jamii.
Katika mahojiano maalumu na TRT Afrika, Msajili wa Jumuiya za Kiraia katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ya nchi hiyo, Emmanuel Kihampa amesema kuwa mchakato huo unalenga kuvifanya vyama hivi viwe vya kihalali ili vipate kinga za kisheria.
Zoezi hili ni zuri, halina hila wala sababu yoyote iliyojificha wala halina nia ya kuingilia watu wala kuminya watu; tunachoangalia hapa ni ustawi na wananchi wetu kwa maendeleo mapana ya taifa letu
Kulingana na Kihampa, mchakato huo haujalenga makundi ya mitandaoni, maarufu kama Whatsapp, kama ilivyodaiwa mwanzoni.
Kwahiyo, ufafanuzi ni kwamba, sisi hatusajili makundi ya Whataspp kwa sababu yale ni majukwaa ya mawasiliano; katika mitandao, kwa hiyo utaratibu wake uko kivingine kabisa na uko chini ya mamlaka na sheria zingine kabisa, sisi tunasajili vyama vilivyoko kwenye jamii…wale walioko kwenye majukwaa hayo, wanaweza kuunda vikundi rasmi, na wakaja kwetu kupata usajili
Msajili huyo amesisitiza kuwa mchakato ni sehemu ya utekelezwaji wa Sheria za mabadiliko ya Sheria Mbalimbali namba 3 ya mwaka 2019, kifungu cha 40, ambacho kinaweka marufuku kwa "kikundi chochote kisichosajiliwa kuendelea kuendesha shughuli zake".
Vivyo hivyo, kifungu cha 41 katika sheria hiyo hiyo kinasema kuwa :“Chama kitakachokuwa kinajiendesha pasipo usajili kinatenda kosa kisheria”.
Kihampa amesisitiza kwamba Serikali ya Tanzania ina malengo mazuri kupitia mchakato huo, ili kuvifanya vyama hivyo viwe vya kihalali kisheria na sio kuviadhibu.
"Tuna nia ya kuona vyama hivi vikipata kinga za kisheria, lakini kutoa hakikisho la ulinzi wa mali na fedha za vyama na kuiwezesha serikali kujua idadi halisi ya hivyo vyama au vikundi, pamoja na mtawanyiko wake nchini", amesema.
Msajili huyo wa Jumuiya za Kiraia anasema kuwa serikali imelenga kuviwezesha vyama hivi kupata wadau wa ndani na nje ya nchi, waweze kupatiwa semina na mafunzo ya kuongeza tija kwenye shughuli zao za kila siku.
Kihampa amesema kuwa ofisi yake imewahi kusajili kikundi kinachokutanisha askari waliopigana vita kuu ya pili ya dunia ambao hukutanika na kuzungumza na kubadilishana mawazo.