Kuanzia asubuhi siku ya Jumanne huduma ya malipo ya pesa kutumia simu, M-Pesa, nchini Kenya iliripotiwa kuwa haifanyi kazi.
M-Pesa ni huduma ya kutuma na kupokea pesa kupitia simu ya mkononi ambayo inaendeshwa na kampuni ya simu ya Safaricom.
Wateja wengine wa kampuni ya simu ya Safaricom walipokea ujumbe unaosema,
"Mpendwa mteja, M-Pesa kwa sasa inafanyiwa matengenezo na haiwezi kushughulikia ombi lako. Tunaomba radhi kwa usumbufu uliojitokeza.”
Huduma ya M-Pesa ikizimika hata kwa dakika chache ni hasara kwa watu wengi nchini Kenya na nje ya nchi. Hii ni kwa sababu huduma hiyo imekuwa tegemeo la watu wengi katika kufanya miamala binafsi na ya kibiashara.
"Leo hii watoto wanarudi shule, tunafaa kulipa karo kwa kutumia M-Pesa, lakini sasa hatuwezi kwa sababu haifanyi kazi. Sasa kwa wale ambao shule inahitaji waingie na karo siku ya kwanza tuko taabani," anasema Joyce Kendi mkazi wa mji wa Nakuru nchini Kenya.
Caroline Njeri ana mtoto wa miaka mitano ambaye anaanza shule leo, anasema, "Hii M-Pesa kutofanya kazi inatusumbua sana, mtoto wangu nilifaa nimnunulie mahitaji ya shule leo ili aanze masomo, lakini sasa inabidi aende bila, akiba yangu yote ya pesa iko M-Pesa," amesema Njeri.
Nazo huduma za serikali pia inabidi zisimamame kwani kuna malipo ambayo hufanywa kupitia M-Pesa.
"Kwa kuwa huduma zote za serikali sasa ziko kwenye nambari moja ya malipo ya M-Pesa, (Paybill) je, hilo si jambo la kusumbua sana nyakati kama hizi wakati M-Pesa iko chini?" @MwangoCapital jukwaa maarufu la uchambuzi wa kiuchumi limeandika katika mtandawo wa X.
Malipo kupitia njia ya kielektroniki hivi sasa yameshika kasi katika maeneo mbalimbali ya Afrika Mashariki. Wengi wanahisi mfumo huo ni salama zaidi.
"Katika mwaka wa 2023, tuliendelea kuwekeza, na kuendeleza uvumbuzi wa bidhaa mpya, tulipoongeza utoaji wa huduma zetu kwa wateja, na miamala ya bilioni 21, yenye thamani ya KShs 35.9 trilioni, iliyopitishwa kupitia jukwaa la M-Pesa," kampuni ya Safaricom imeonyesha katika ripoti yake ya mwaka 2023.
M-Pesa ina wateja zaidi ya milioni 56 wanaoitumia na hivyo kuimarisha nafasi yake kama jukwaa kubwa zaidi la malipo ya kiteknolojia barani Afrika.
Lakini si Kenya tu, ambayo imeathiriwa kwa kusimamishwa kwake kwa muda. M-Pesa iliyozinduliwa zaidi ya miaka 14 iliyopita sasa inapatikana nchini Tanzania, Msumbiji, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Lesotho, Ghana na Misri.
Nchini Kenya wananchi wameonyesha kutofurahia kwao kwa kampuni ya Safaricom huku wengine wakipokea ujumbe huu:
"Samahani kwa usumbufu uliojitokeza. Tunakumbana na hitilafu ya kiufundi na mfumo wa M-PESA na azimio linaendelea kutoa suluhu, tafadhali kuwa na subira tunaposhughulikia."
"Hivi ndivyo nchi nzima inavyotegemea huduma moja ya uhamishaji pesa iliyojumuishwa kifedha. Wakati M-Pesa iko chini, kila kitu kinaporomoka. Kwa hivyo, haipaswi kuwa chini hata sekunde," amesema Caleb Hamisi, mbunge wa jimbo la Saboti.
Mpaka wakati taarifa hii inaenda hewani, huduma hiyo ya M-Pesa ilikuwa bado haijarudi.