Gen Z wanatangamana kwa usawa na umoja wa dhati. Hawajui cha Kabila, dini, rangi ya ngozi au mali / Picha : Reuters 

Kwa zaidi ya wiki sasa, pilka pilka nchini Kenya imekuwa kati ya polisi wa kukabiliana na ghasia na vijana wanaopinga mswada wa fedha 2024.

Lakini tofauti na maandamano mengine, maandamano haya yanaonekana kuongozwa zaidi na vijana wa umri mdogo wanaofahamika zaidi kama Gen Z.

Pia mtindo wanaotumia kushinikiza maandamano hayo ni tofauti kabisa na ilivyotumika miaka ya nyuma.

Hii imesababisha watu kuwamulika zaidi na kuwazungumzia kuanzia bunugeni hadi vyombo vya habari na mtandaoni.

Basi Gen Z ni kina nani?

Tunaposema Gen Z, au Millenials au Gen X, tunazungumzia kizazi cha watu kati ya umri Fulani. Na huu ni mfumo ambao ulianza kutumiwa Marekani huku kila kizazi kikiambatanishwa na tukio au mfumo wa uongozi na mtindo wa maisha.

Aina mbali mbali za vizazi vinavyotambuliwa

Ili kuelewa Gen Z inabidi kuelewa kuwa wao ni muendelezo wa vizazi vilivyowatangulia ambao kila moj aimepewa jina kutokana n autofauto wao kwa mitindo yao ya maisha, imani zao na umri walipozaliwa.

Kizazi cha GI (1901-1927)

Hiki ni kizazi kinachotajwa kuwa cha kwanza kwa muorodhesho. Walizaliwa kati ya 1901-1927. Kizazi hiki kiliishi kupitia nyakati za kuporomoka uchumi wa dunia na kisha kwenda kupigana katika Vita vya Dunia vya pili. Hasa, walifanya maarufu muziki wa jazz Swing.

Kizazi Kimya (1928-1945)

Kizazi kilicho kimya kilipata jina lao kwa kuwa wenye kutii zaidi utawala na kwamba walinyamaza kimya wakati wa enzi ya Ukomunisti ilipoenea nchini.

Kizazi cha Baby Boom (1946-1964)

Boomers ni jina la idadi ya watu "boom" ambayo ilitokea baada ya vita vya pili vya Dunia na vijana wengi wa kizazi hiki walikaidi wazazi wao, walipinga Vita vya Vietnam, na kuunda "Summer of Love." walianzisha mfumo wa kuwashirikisha watoto wao kwa maamuzi ya kinyumbani.

Kizazi X (1965-1980)

Kizazi cha X ambacho mara nyingi kilitupiliwa mbali kama kizazi chenye ulegevu, kilipitia janga la UKIMWI, utamaduni wa MTV, na mazingira yanayobadilika ambayo yangetoa haki za kibinadamu. Kizazi hiki huhusika zaidi na maendeleo ya kijamii na kielimu ya watoto wao.

Kizazi Y au Millenials ( 1981–1996)

Kizazi hiki pia kilipitia masaibu ya mlipuko wa UKIMWI na pia wana uzoefu wa malezi ya utotoni na bila mtandao, ambao sasa una ushawishi mkubwa katika maisha yao ya kibinafsi. Pia wanatazamiwa kuwa na hamasa juu ya mazingira na haki za binadamu.

Gen Z wana uzoefu zaidi katika mitandao ya kijamii na wanajua kutumia fursa hiyo kujieleza na kutafuta ushawishi nje na ndani ya nchi / Picha : Reuters 

Gen Z (1997-2010)

Vijana wakubwa zaidi katika Gen Z watakuwa katika kuelekea miaka ya mwisho mwisho ya ishirini na wadogo zaidi watakuwa na miaka 12.

Hiki ni Kizazi kilicho na uzoefu zaidi katika masuala ya Teknolojia na hasa mitandao ya kijamii. Tunapozungumzia vijana wa leo, ndio hawa hasa.

Kujihusisha kwao katika siasa kama vile Kenya kumewaamsha bongo wanasaisa wakongwe zaidi maana Gen Z wanachukuliwa kuwa na ushawishi mkubwa na wenye uwezo wa kusukuma ajenda na kuleta mabadiliko wakiamua.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na taasisi ya Pew nchini Marekani Hawa Gen Z wanatangamana kwa usawa na umoja wa dhati. Hawajui cha Kabila, dini, rangi ya ngozi au mali.

Ingawa vizazi vilivyopita vimeshughulikia masuala ya kijamii, Gen Z wana maslahi ya kijamii zaidi kuliko vizazi vilivyotangulia. Wanaangazia maswala saba muhimu ya kijamii: huduma ya afya, afya ya akili, elimu ya juu, usalama wa kiuchumi, ushiriki wa raia, usawa wa rangi na mazingira.

Wengi wao wamechangamka sana katika mitandao ya kijamii na wanajua kutumia fursa hiyo kujieleza na kutafuta ushawishi nje na ndani ya nchi.

Kwa kuwa hawana mshikamano wa kisiasa, mara nyingi ajenda zao ni za utaifa kwa jumla na hawashawishiki kwa urahisi.

TRT Afrika