Gavana wa kieneo nchini Kenya amekamatwa kuhusiana na mapigano ya koo katika kaunti ya Tana River pwani ambapo watu kadhaa wameuawa.
Dhadho Godhana, pamoja na mbunge wa eneo hilo, walikamatwa kila mmoja kivyake kwa kukosa kuheshimu wito kuhusiana na mapigano hayo, polisi walisema Jumamosi. Wawili hao hawajajibu hadharani shutuma hizo.
Takriban watu 14 wameuawa katika mapigano yaliyotokea kusini-mashariki mwa Kenya, na kusababisha mamlaka kutaja maeneo mawili katika kaunti hiyo kuwa hatari na ukosefu wa usalama kwa siku 30 zijazo.
Usalama umeimarishwa katika maeneo hayo na wakaazi wamepigwa marufuku kubeba silaha, kulingana na notisi ya gazeti la serikali ya wizara ya mambo ya ndani.
Gavana ahojiwa
Godhana alijiwasilisha Jumamosi asubuhi katika makao makuu ya Kurugenzi ya Upelelezi wa Jinai (DCI) katika mji mkuu, Nairobi, na alikuwa akihojiwa kuhusu mapigano hayo, mkuu wa DCI Mohamed Amin alisema.
"Tunatazamia kuwashtaki wale ambao watapatikana na hatia kuhusu kile kinachoshuhudiwa Tana River, tutakapomaliza uchunguzi," alinukuliwa akisema na tovuti ya habari ya Citizen.
Wanasiasa watano kutoka kaunti ya Tana River tayari wametakiwa kufika mbele ya Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC) Jumatatu kuhojiwa kuhusu madai ya kuchochea migogoro kati ya jamii mbili.
Tana River hapo awali ilishuhudia mapigano ya kikabila kuhusu haki ya malisho ya ng'ombe ambayo yalisababisha vifo vya watu kadhaa.