Gavana wa Kaunti ya Kisumu nchini Kenya, Anyang' Nyong'o, leo ametoa wito kwa Bidco Oil Refinery kuacha shughuli zote za kibiashara na Israel.

Katika taarifa ya vyombo vya habari iliyotolewa jioni siku ya Jumatatu, 19 Feb, Profesa Nyong'o alisema kuwa alikuwa akiitaka Bidco kujizuia kuchukua hatua hii kwani inakwenda kinyume na maamuzi yaliyofanywa hivi karibuni na Umoja wa Mataifa na Mahakama ya Kimataifa ya Haki, ICJ.

"Nimegundua kwa wasiwasi uamuzi uliofanywa na moja ya kampuni kubwa zaidi za Kenya, viwanda vya mafuta vya Bidco kufanya mikataba ya kibiashara na Israel, nchi inayokabiliwa na laani kwa mashambulizi yake ya damu dhidi ya Wapalestina." taarifa hio inasema.

Profesa huyo aliendelea kusema kuwa mashambulizi ya anga yameua zaidi ya Wapalestina 25,000 huku watu milioni 1.9 wakiwa wamehamishwa kutoka makazi yao.

Alisistiza kuwa suluhisho pekee ni njia ya mataifa mawili katika kutatua mgogoro kati ya Israel na majirani zake.

TRT Afrika