Sekunde 20 tu baada ya kipenga Gambia walikua tayari ndani chumbani kwa Honduras kupitia mkwaju uliofungwa na Adama Bojang kutoka mbali.
Uwanja mzima wa Mendoza ukasisimka wakijua leo ni leo.
Nao Honduras wakajibu shari kwa shari walipotikisa wavu wa Gambia dakika nne baadaye kupitia mshambuliaji Marco Aceituno aliyefikisha nyumbani pasi kutoka kwa Isaac Castillo.
Mechi haikutulia kamwe na mashabiki waliachwa juu juu huku tishio baada ya tishio timu zote mbili zikipelekana hadi nusu fainali.
Nusu ya pili Gambia walicheza kama wao na kuonesha kwanini mwaka huu wamefuzu kombe hili kwa mara ya kwanza.
Kuelekea kumalizika mechi Mara Bojang akatimuka tena na kutikisa wavu wa Honduras kwa bao lake la pili dakika ya 84. Honduras kama vile wakaona wamemulikwa tochi nao wakafyatua dakika nne tu baadaye ila lao likakataliwa kutokana na kuwa Daniel Carter alikuwa ameotea.
Ila kibarua sasa kipo Gambia wanapokutana na Ufaransa katika mechi yao ya kundi F, Alhamisi.
Kwa upande wake Tunisia walipigwa 1-0 na Uiengereza katika mechi yao ya ufunguzi ya kundi E. Dane Scarlet aliipatia nchi yake bao la pekee katika mechi hiyo dakika ya 25.
Ulinzi wa timu ya Uingereza ulionekana kupewa kibarua kigumu na Mshambuliaji wa Tunisia Bechir Yacoud japo nao waliamua kumkaba asipite popote.
Tunisia watakutana na Iraq Alhamisi katika mechi yao ya pili la kundi E.