Wengi wao walikuwa chini ya umri wa miaka mitano na sasa wataalam wa tiba na dawa wameanza kuhoji usalama wa dawa za watoto kuzuia kukohoa, ikizingatiwa kuwa wazazi wengi barani Afrika wanapendelea kwenda katika maduka ya kuuza dawa mara pindi tu watoto wao wanapoanza kuugua sema; labda kukohoa au joto mwilini kuongezeka.
Madkatari sasa wameshauri kutonunua dawa za kuzuia kukohoa katika maduka kwani uchunguzi umebaini hazina suluhu la kudumu.
“Binafsi mimi sishauri mzazi kununua dawa za kuzuia kukohoa kwani ushahidi kuwa zinasaidia kutibu tatizo kabisa ni finyu sana. Nashauri kutumia asali na limau kama tiba mbadala,” anasema Emmanuel Agogo, ambaye ni mtaalamu wa tiba nchini Nigeria.
Shirika la afya duniani WHO tarehe 5 Oktoba lilishauri kutotumika kwa dawa nne kutokana kiwango kikubwa cha kemikali ya diethylene glycol(DEG) na ethylene glycol(EG). WHO iiziorodhesha dawa hizo kuwa -- Promethazine Oral Solution, Kofexmalin Baby Cough Syrup, Makoff Baby Cough Syrup na Magrip N Cold Syrup – zote ziligundulika kuwa na viwango hatari vya DEG na EG.
“Vipimo vilivyofanyika vilionesha kuwa dawa hizo zilikuwa na takriban asilimia 19 ya DEG wakati kiwango kinachostahili ni asilimia 0.1 pekee,” anaeleza Daktari Peter Adebayo Adewuyi kutoka Gambia.
“Kiwango cha DEG kilichoko katika dawa hizo hakistahili kabisa,” anaeleza TRT World.
Kwa takriban karne moja utafiti umeonesha kuwa DEG – ambayo ni kemikali zito yenye sukari inaweza kusababisha vifo vya atu wengi kama ilivyofanyika nchini Gambia. Aidha viwango vingi vya DEG vinaweza kusababisha kufeli kwa figo na mgonjwa akafariki dunia ndani ya siku chache tu.
Maafa yaliyotokana na DEG
Kisa cha kwanza cha watu kufa kutokana na kemikali ya DEG kilifanyika mwaka wa 1937 nchini Marekani wakati dawa ya kuzuia bakteria ijulikanayo kama Elixir of Sulfanilamide iliwasili sokoni. Takriban watu 105, miongoni mwao watoto 34, waliaga dunia ndani ya siku chache baada ya matumizi.
Hali hiyo ilipelekea serikali ya Marekani kutunga sheria iliyoruhusu FDA kuchunguza dawa zote kabla ya kuingia sokoni kuuziwa wananchi.
Kemikali ya DEG mara nyingi hutumika katika viwanda vya kutengeneza bidha kama maji ya breki, wino na vipodozi.
Baadhi ya kampuni za kutengeneza dawa huitumia kimakosa ama kwa maksudi kama mbadala wa Polyethene glycol(PEG) ili kupunguza gharama aya utengenezaji.
“Wahalifu wanaweza tengeneza faida kubwa kwa kutumia DEG badala ya PEG,” anasema Daktari Joel Selanikio kutoka Marekani, ambaye pia anafanya kazi na Shirika la afya dunia WHO.
Aidha zaidi ya watu 100 waliaga dunia kutokana na dawa zenye viwango vingi vya DEG nchini Panama mwaka 2006. Dawa za aina hiyo ni nyingi na zipo kila mahali katika maduka ya kuuza dawa.
“Hali halisi barani Afrika ni kuwa wauza-dawa madukani ndio wanaotoa ushauri kwa wagonjwa juu ya matumizi ya dawa hizi.” Anasema Agogo.
Serikali ya India imetoa maelezo kuwa dawa hizo zilikuwa zimetengenezwa kwa ajili ya soko la Gambia lakini hatahivyo WHO imeonya kuwa huenda pia zimefikia mataifa mengine.
Udhibiti finyu
Kampuni ya dawa ya Maiden Pharmaceuticals iliyoko Haryana India sio geni katika visa kama hivi vya kusababisha vifo nchini Gambia. Kampuni hiyo-hiyo ilipigwa marufuku katika jimbo la Bihar nchini India kwa kuuza dawa zisizokidhi vigezo . Aidha imepigwa marufuku kuuza dawa zozote nchini Vietnam kwa mujibu wa ripoti nchini India.
Maiden wamesema kuwa wamestushwa na kilichotendeka nchini Gambia na WHO kwa ushirikiano na serikali ya India wameanzisha jalada la uchunguzi kubaini ni kipi hasa kilipelekea kuwekwa kwa viwango hatari vya DEG kwenye dawa.
“Vipo vifaa vinavyoweza kubaini tofauti kati ya DEG na PEG iwapo vitatumika ipasavy,” anasema daktari Selaniko.
“Hakuna kampuni yenye heshima inayoweza kuweka viwango hatari vya DEG kwenye dawa na ikitokea basi wamefanya hivyo, lazima kuna utepetevu mkubwa na udhibiti finyu wa kupima DEG.”
Mara nyingi udhibiti hafifu kutoka kwenye viwanda ndiyo chanzo cha matatizo yoye haya.
Serikali ya Gambia vilevile imekosolewa pakubwa kwa kufeli kuchunguza dawa zinazoingizwa na kuuzwa kwenye maduka ya dawa.
TRT haikufanikiwa kumpata Markieu Janneh Kaira, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa bodi ya uchunguzi wa dawa nchini Gambia, licha kumtumia maombi ya mahojiano naye mara kadhaa.