Polisi nchini Zimbabwe inaendelea kuchunguza tukio hilo./Picha: AFP

Jeshi la Polisi nchini Zimbabwe linamshikilia mtu mmoja aliyejitambulisha kama nabii , pamoja na kugundua makaburi mapya 16, yakiwemo ya watoto wachanga. Jeshi hilo, pia limegundua zaidi ya watoto 250 waliokuwa wakitumikishwa.

Katika taarifa, msemaji wa Jeshi la Polisi la nchi hiyo Paul Nyathi anasema Ishmael Chokurongerwa, mwenye miaka 56, anaongoza kikundi cha wafuasi zaidi ya 1,000 wanaokutana katika shamba maalumu, lililoko takribani kilomita 34, kaskazini magharibi mwa mji mkuu wa nchi hiyo, Harare.

Kulingana na Nyathi, watoto hao walikuwa wanatumikishwa katika shughuli ngumu kwa manufaa yake mwenyewe. Kati ya watoto 251, 246 hawakuwa na vyeti vya kuzaliwa.

“Polisi wamegundua kuwa watoto hao wenye umri wa kwenda shule, hawakupata elimu rasmi na walitumikishwa kwenye kazi ngumu,” anasema Nyathi.

'Vitendo vya kihalifu'

Kati ya makaburi hayo, saba yalikuwa ni ya watoto wachanga ambao vizazi vyao havikuwa vimesajiliwa.

Kulingana na Nyathi, maofisa polisi walivamia eneo hilo siku ya Jumanne. Chokurongerwa, anayejiita Nabii Ishmael alikamatwa akiwa na wasaidizi wake kwa kuendesha matukio ya uhalifu dhidi ya watoto.”

Nyathi amesema taarifa zaidi juu ya uchunguzi wa tukio hilo unaendelea na utatolewa ndani ya siku chache.

Gazeti la H-Metro, ambalo lilikuwa sehemu ya operesheni hiyo, walionesha picha za polisi waliovalia mavazi maalumu, wakibishana na waumini wanawake waliokuwa wakishinikiza kuchukua watoto wao waliokuwa wamewekwa kwenye basi la polisi. Haikufahamika mapema sababu ya polisi kuwazuia watoto hao.

'Hakuna elimu'

“Kwanini wanawachukua watoto wetu? Tumeridhika kuwepo hapa. Hatuna tatizo lolote,” alilalamika mwanamke mmoja kupitia video mjongeo iliyowekwa kwenye mtandao wa X.

Kulingana na gazeti hilo, polisi walikuwa na silaha, mabomu ya machozi na mbwa walivamia eneo hilo la makaburi ambalo wanaliita kama "nchi yao ya ahadi."

Mmoja wa wasaidizi wa Chokurongerwa alifanyiwa mahojiano na gazeti hilo.

“Imani yetu haitoki kwenye maandiko, tumeipata moja kwa moja kutoka kwa Mungu aliyetupa sheria za kuingia mbinguni. Mungu anakataza elimu kwani yanayofundishwa yanakwenda kinyume na maagizo yake,” alisema, na kuongeza “Mungu alituambia mvua haitonyesha kama tutawapeleka watoto wetu shule. Ona hali ya ukame ilivyo, na sisi tunapata mvua hapa. Tumepata zawadi ya sikio la kiroho ya kusikiliza sauti ya Mungu,” alisema.

'Kushinda njaa mpaka kifo'

Makundi ya kitume ambayo yanaingiza imani za kimapokeo katika fundisho la Kipentekoste ni maarufu katika nchi hiyo ya kusini mwa Afrika yenye kidini.

Kumekuwa na utafiti mdogo wa kina kuhusu makanisa ya Kitume nchini Zimbabwe, lakini tafiti za UNICEF zinakadiria kuwa ndilo dhehebu kubwa zaidi la kidini lenye wafuasi karibu milioni 2.5 katika nchi yenye watu milioni 15. Baadhi ya vikundi hivyo vinazingatia mafundisho yanayowataka wafuasi kuepuka elimu kwa watoto wao pamoja na dawa na huduma za matibabu kwa wanachama ambao wanapaswa kutafuta uponyaji kupitia imani yao katika sala, maji matakatifu na wapakwa mafuta.

Katika miaka ya hivi karibuni, baadhi yao wamewaruhusu wafuasi wao kutembelea hospitali na kuwaanzisha watoto wao shule, kufuatia kampeni mfululizo kutoka serikalini na taasisi zisizo za kiserikali.

Aprili mwaka jana, Kenya ilimkamata mchungaji aliyesemekana kuwalazimisha wafuasi wake washinde njaa ili waweze kumuona Yesu.

Mwendesha mkuu wa Mashitaka wa nchi hiyo aliagiza mchungaji Paul Mackenzie na wenzake 90 washitakiwe kwa mauaji ya wafuasi wao 429, ukatili na utesaji.

TRT Afrika