Gambia imeiacha Ufaransa kinywa wazi baada ya kuipiga mbati 2-1, kombe la dunia U-20

Gambia imeiacha Ufaransa kinywa wazi baada ya kuipiga mbati 2-1, kombe la dunia U-20

Timu za Afrika za Gambia na Tunisia zimeibuka washindi katika mechi zao ya Alhamisi, na kupenya kwa raundi ya mchujo.
Gambia wameendeleza ushindi wao katika awamu ya makundi kombe la dunia  U-20 / Photo: AFP

Adama Bojang, aliwasha moto kwa timu yake alipofyatua kombora lililopanguliwa na kipa japo kwa bahati nzuri au mbaya mpira ukamgonga beki wa Ufaransa Tanguy Zoukrou na kupenya wavuni, na hivyo kuwapa Gambia uongozi dakika ya 13.

Ufaransa walifanikiwa kusawazisha kupitia Wilson Odobert dakika ya 61 japo sherehe zao zilizimwa dakika tano baadaye na Mamin Sanyang alipotikisa wavu wa Ufaransa na kuihakikishia timu yake nafasi katika awamu ya mchujo.

Gambia wamepenya wakiwa wamesalia na mechi moja kucheza huku Ufaransa wakiachwa hoi katika hatari ya kung’olewa.

Tunisia wamefanikiwa kujikomboa katika mechi yao ya pili awamu ya makundi, nakujiongezea matumaoini ya kupenya raundi ya mchujo Picha : Reuters

Tunisia waliingia mechi ya Alhamisi wakiwa na hasira wakitaka kulipiza kichapo walichopata mechi yao ya kwanza ya makundi dhidi ya England.

Mpira uliitika walipo wakanyanga Iraq 3-0 katika mechi iliyojaa msisimko.

Iraq walitawala mechi katika nusu ya kwanza licha ya kutofunga bao na kuwatoa kijasho Tunisia. Hata hivyo mambo yaligeuka waliporudi uwanjani kipindi cha ya pili.

Tunisia waliwafunga wairaqi bao baada ya bao na kuwaacha na mshangao. Hii ni mara ya kwanza kwa Tunisia kufungwa zaidi ya bao moja katika mchuano huu. Iraq wamefungwa mechi zao zote na hivyo kusalia chini ya jedwali.

Katika mechi ya awali, Nigeria waliwapiku waitalia na kujishindia alama kamili za makundi kwa kuwalaza 2-1.

Nigeria na Gambia wameshajihakikishia nafasi katika raundi ya mchujo huku Senegal na Tunisia wakiendelea kupigania kujikomboa.

TRT Afrika