ALi Bongo

Na

Sylvia Chebet

Mgogoro wa sasa wa kisiasa nchini Gabon ulizuka huku Ali Bongo Ondimba, 64, akitangazwa mshindi wa uchaguzi wa urais wa Agosti 26 alipokuwa akitafuta muhula wa tatu madarakani kwa miaka saba.

Bongo alimshinda mpinzani wake mkuu Albert Ondo Ossa katika duru moja ya kura, na kujikusanyia 64.27% ya kura, kulingana na matokeo ya baraza la uchaguzi.

Mwanasiasa huyo alikuwa akitafuta kupanua ushawishi wa kisiasa wa familia yake iliyoshikilia madaraka kwa miaka 55 nchini Gabon. Bongo aliingia madarakani mwaka 2009 baada ya kifo cha baba yake, Omar Bongo Ondimba, ambaye alitawala nchi hiyo kwa miaka 42 tangu 1967.

Lakini baada ya miaka 14 kama rais, muhula wa tatu wa Bongo uko kwenye matata. Baadhi ya wanajeshi walitangaza mapema Jumatano asubuhi kwamba walichukua madaraka.

Kupanda madarakani

Baada ya kifo cha baba yake mwaka wa 2009, Bongo alishinda uchaguzi wa urais uliofuata mwaka wa 2011 huku kukiwa na madai ya udanganyifu. Kuhesabiwa upya kwa kura bado kunaifanya Bongo kuongoza kwa asilimia 41.79 ya kura. Mnamo 2016, alishinda muhula wake wa pili kwa tofauti ndogo huku kukiwa na maandamano ya vurugu.

Huku Bongo akiwania muhula wa tatu madarakani katika uchaguzi wa wiki jana baada ya mabadiliko ya katiba yaliyomruhusu kufanya hivyo, upinzani uliungana kumuunga mkono mpinzani wake mkuu, profesa wa uchumi Albert Ondo Ossa.

Wakati wa utawala wa babake, Bongo aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje kuanzia 1989-1991 kabla ya kuuuwakilisha mji aliokozaliwa wa Bongoville akiwa mbunge katika Bunge la Kitaifa kwa miaka minane kuanzia 1991-1999.

Baadaye, aliteuliwa katika wadhifa mwingine wa uwaziri, kama waziri wa ulinzi, ambapo alihudumu kwa miaka 10 kutoka 1999 hadi 2009 wakati baba yake alikufa.

Familia ya Bongo

Familia yake ilisilimu mwaka wa 1973, mabadiliko ambayo yalibadilisha majina yao. Alizaliwa Alain Bernard Bongo, Februari 9, 1959, huko Congo Brazzaville kisha akawa Ali Bongo Ondimba.

Ali Bongo Ondimba alizaliwa Alain Bernard Bongo lakini alibadilisha majina baada ya kusilimu. Picha: Nyingine

Jina la baba yake awali lilikuwa Albert Bernard Bongo lakini baadae likabadilishwa na kuwa Omar Bongo Ondimba. Mama yake, Patience Dabany ni mwanamuziki wa zamani na malkia wa urembo.

Bongo alipokuwa na umri wa miaka tisa, alipelekwa katika shule ya kibinafsi huko Neuilly, Ufaransa.

Mnamo 1978, Bongo ilirekodi albamu ya funk yenye jina A Brand New Man, iliyotayarishwa na Charles Bobbit, meneja wa James Brown, na yenye sauti za nyuma na muziki wa bendi ya Brown. Wimbo wa kwanza kutoka kwa albamu hiyo ulikuwa "I Wanna Stay With You."

Bongo alisomea sheria na kuhitimu kutoka Pantheon-Sorbonne huko Paris mnamo 1978, na akapokea udaktari kutoka Chuo Kikuu cha Wuhan nchini China mnamo 1980.

Bongo alioa mke wake wa kwanza Sylvia Valentin, raia wa Ufaransa, mwaka 1989, na wanandoa hao wana watoto wanne.

Alioa mke wake wa pili, Inge Collins, wa Los Angeles, California, mnamo 1994 lakini Collins aliwasilisha kesi ya talaka mnamo 2015.

Safari ndefu

Ali Bongo alijihusisha na siasa mwaka wa 1981 alipojiunga na chama cha Gabon Democratic Party (PDG). Mnamo 1983 alichaguliwa kwa Kamati Kuu ya PDG, na kumfanya kuwa mjumbe wa baraza la mawaziri la baba yake.

Punde si punde akawa mwakilishi wa kibinafsi wa baba yake na akashika wadhifa wa Mwakilishi Mkuu wa Kibinafsi wa Jamhuri kutoka 1987 hadi 1989. Marekebisho ya katiba ambayo yaliweka sharti la umri wa miaka 35 kwa mawaziri lilisababisha kuondoka kwake.

Akiwa mwakilishi wa Bongoville katika Bunge la Kitaifa, alikua Rais wa Baraza la Juu la Masuala ya Kiislamu la Gabon mnamo 1996, na Waziri wa Ulinzi mnamo 1999.

Bongo alipatwa na kiharusi Oktoba 2018, alipokuwa akihudhuria kongamano la kimataifa mjini Riyadh, Saudi Arabia.

President Ali Bongo Ondimba on a visit to Equitorial Guinea

Muda mfupi baadaye mnamo Januari 2019, alipata shida nyingine. Mapinduzi yalifanywa dhidi yake lakini hayakufaulu. Aliendelea kutangaza kwamba atagombea tena uchaguzi wa 2023.

Uchaguzi huo ulifanyika Agosti 26 na tume ya uchaguzi ilimtangaza mshindi Agosti 30. Lakini wanajeshi walitangaza kufuta matokeo, walichukua mamlaka na kumweka katika kizuizi cha nyumbani.

TRT Afrika