Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Felix Tshisekedi ameshinda muhula wa pili kwa kishindo, hayo ni kwa mujibu wa matokeo ya kwanza ya Tume ya Uchaguzi. Hata hivyo, upinzani unasema uchaguzi huo ulikuwa na kasoro.
Matokeo ya kwanza katika kura ya urais, yaliyotangazwa na kamishna wa Tume ya Uchaguzi nchini humo CENI, yameonyesha Tshisekedi ameshinda kwa asilimia 73 ya kura.
Moise Katumbi — mfanyabiashara tajiri, na mmiliki wa klabu ya mpira na aliyekuwa gavana, alifuatia kwa asilimia 18.
Mahakama ya Katiba ya nchi hiyo inatarajiwa kuthibitisha matokeo hayo tarehe 10 Januari.
Tshisekedi, 60, aliingia madarakani kwa mara ya kwanza, Januari 2019, baada ya uchaguzi uliopingwa ambao waangalizi wanasema alishindwa.
Martin Fayulu, ambae anasema ameibiwa kura ya urais ya uchaguzi wa 2018, pia alishiriki katika uchaguzi uliopita, lakini aliambulia asilimia 5 tu ya kura.
Wagombea 20 waliosalia, akiwemo Denis Mukwege, mshindi wa tuzo ya Nobel aliyoipata kutokana na mchango wake kwa wanawake waathirika wa vitendo vya unyanyasaji wa kingono, hakuzidisha wala kupunguza asilimia moja.
Wagombea tisa wa upinzani miongoni mwao, Mukwege, Fayulu na Katumbi — Jumapili walisaini tamko la kile walichokiita, 'uchaguzi uliogubikwa na kasoro' na kutaka uchaguzi urudiwe.
Fayulu, akizungumza na waandishi wa habari katika mji wa Kinshasa siku hiyo hiyo, amesema matokeo "yamechezewa. Hii haikubaliki."
Tresor Kibangula, mchambuzi wa siasa katika kituo cha Utafiti cha Ebuteli, ambae amezungumza na AFP kabla ya kutangazwa kwa matokeo kamili, amesema, idadi ya kura ya Tshisekedi "ni zaidi ya matarajio ya watu."
"Kampeni yake imefanya kazi," lakini matokeo yake katika baadhi ya majimbo, "yanaibua maswali kuhusu athari za kasoro ambazo zimeonekana."