Felix Tshisekedi ni rais wa kwanza kuchukua hatamu ya uongozi kupitia njia ya kidemokrasia tangu Jamhuri hiyo ya Kidemokrasia ya Kongo kujinyakulia uhuru 1960.
Tshisekedi, aliye na miaka 60, ni mtoto wa kati katika familia ya watoto watano, ni mrithi wa kisiasa wa marehemu baba yake Étienne Tshisekedi, aliyekuwa mwanasiasa mkongwe nchini DRC.
ÉtienneTshisekedi wa Mulumba alianzisha chama cha 'Union Pour la Démocratie et le Progrès Social' (UDPS), mnamo1982, kilichokuwa chama cha Upinzani kupinga utawala wa Mubutu Sese Seko aliyekuwa madarakani wakati huo.
Harakati za kisiasa za Tshisekedi 'mkubwa' zilimpelekea kuwekwa korokoroni mara nyingi na hivyo basi familia kulazimika kuhama Kinshasa na kwenda kujificha katika kijiji chao cha asili katika eneo la Kassai.
Hata hivyo, hiyo haikuwa dawa kwani masaibu yaliendelea kuwaandama.
Mnamo 2011, Étienne Tshisekedi alichaguliwa kuwa mbunge wa jimbo la Mbuji-Mayi katika eneo la Kassai. Mwaka huo, Baba yake Étienne alishindwa uchaguzi na aliyekuwa rais wa nchi hiyo Joseph Kabila.
Mzee Étienne Tshisekedi alifariki dunia tarehe 1 Februari 2017 nchini Ubelgiji na kuzikwa miaka 2 baadaye.
Baada ya kifo cha baba yake mnamo 2017, Tshisekedi mtoto alirithi chama kilichoongozwa na babake cha 'Union pour la Démocratie et le Progrès Social' UDPS.
Alilikumbatia jukumu hilo kikamilifu na hata kujijengea safari ya kisiasa na kuwa mgombea urais kupitia chama hicho kwenye uchaguzi wa urais wenye utata mnamo 2018.
Kufuatia makubaliano ya mwaka 2017 kati ya serikali na upinzani maarufu ''Accords de Saint Sylvestre,'' jina lake lilitajwa kuwa na uwezekano wa kushililia wadhifa wa waziri mkuu, lakini hatimae rais wa kipindi hicho Joseph Kabila alimchagua Bruno Tshibala.
Hata hivyo, Felix Tshisekedi hakuvunjika moyo kwani aliendeleza na harakati zake za kisiasa na kuchukua uongozi kamili wa chama cha UDPS na hata kuwa mgombea wa Chama kwenye kinyanganyiro cha uchaguzi mkuu wa 2018.
Felix Tshisekedi alishinda uchaguzi wa urais kwa kupata asilimia 36 ya kura na kutawazwa mshindi mnamo tarehe10 Januari 2019 kuwa rais wa tano wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Tshisekedi alihudumu muhula wa kwanza ingawa kipindi chenyewe kilikumbwa na migogoro ya kivita na kisiasa hasa eneo lake la mashariki.
Mnamo 2021, Tshisekedi alichaguliwa mwenyekiti wa AU katika kikao cha kawaida cha 34 kilichofanyika kati ya tarehe 6-7 Februari na kuchukua nafasi ya rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa.
Akiwa na umri wa miaka 22, Felix Tshisekedi pamoja na mama yake na ndugu zake, walipata hifadhi mjini Brussels, nchini Ubelgiji na hapo ndipo alipopachikwa jina lake la Utani la ''Fatshi'' ambalo anafahamika nalo hadi leo.
Tshisekedi 'akajiunga' na Chuo Kikuu na kusoma katika Kitivo cha Masoko na Mawasiliano.
Tsishekedi ameingia uchaguzi uliomalizika wa DRC wa Disemba 20 na kauli mbiu ya kurudisha hadhi na uhuru wa DRC ikiwemo kupambana na makundi yote ya waasi kama vile M23.