Mwili wa mpandaji wa mlima kutoka Kenya, Cheruiyot Kirui, aliyefariki wakati akijaribu kufikia kilele cha Mlima Everest bila oksijeni, utabaki kwenye mlima huo mrefu zaidi duniani, kulingana na familia yake.
Kulingana na taarifa iliyoandikwa na rafiki yake wa karibu James Muhia, familia yake haikutaka kuhatarisha maisha ya mtu yeyote kwa kujaribu kuurudisha mwili wake kutoka kwenye ufa alioangukia, ambao ulikuwa takriban mita 48 kutoka sehemu ya juu kabisa duniani.
"Cheruiyot alianguka kwenye ufa mita 48 kutoka kilele (mita 8,848) na kuurejesha mwili wake kutoka huko juu itakuwa hatari kwa timu ya uokoaji, familia haitaki kuhatarisha maisha ya mtu yoyote," taarifa ya Jumatano kwa vyombo vya habari inasomeka.
"Cheruiyot alikuwa na upendo wa dhati kwa milima, na milima pia ilimpenda. Tunapata faraja kwa kujua anapumzika katika sehemu aliyofurahia."
Familia pia ilitoa rambirambi kwa familia ya Nawang, Sherpa (mbeba mizigo na mwongoza njia) wa Cheruiyot katika safari hii, ambaye bado hajapatikana.